2015-12-21 15:41:00

Papa: Onesheni upendo kwa kuwajali wenzi wenu wa ndoa na watoto!


Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 21 Desemba 2015 baada ya kuwatakia heri na baraka za Siku kuu ya Noeli wasaidizi wake wa karibu, ambao amewataka kuzingatia fadhila kumi na mbili, zitakazowasaidia kutekeleza wajibu wao kikamilifu, huku wakiambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha, alikutana na wafanyakazi wote wa Vatican wakiwa pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya hata pale ambapo kazi hizi zimekuwa hazina mabadiliko.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa Vatican kuwa na ari na moyo mkuu wa kuendelea kutekeleza nyajibu zao katika maeneo mbali mbali ya kazi kwa kushirikiana, kwa uvumilivu na kusaidiana. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii pia kuomba msamaha kutokana na kashfa mbali mbali ambazo zimejitokeza hivi karibuni mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika wafanyakazi hawa na familia zao, kuwaombea wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na kashfa hizi, ili waweze kupata mwelekeo sahihi wa maisha.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa Vatican kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa familia na watoto wao kwa kutambua kwamba, ndoa ni kama mti mwororo unaopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Zawadi kubwa ambayo watoto wanaweza kupokea kutoka kwa wazazi wao ni upendo, kumbe ni wajibu wa wazazi kuonesha upendo wa dhati, ili watoto wao waweze pia kufurahia maisha. Wanandoa walinde na kutunza ndoa kwa kuboresha mahusiano yao kila siku. Kipaumbele cha kwanza ni kwa utu wa mtu na wala si vitu anakaza kusema Baba Mtakatifu.

Familia zao ziwe kweli ni chemchemi ya huruma ya Mungu, kwa kuwahudumia wazee na wagonjwa, ili kweli Familia iweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yaguse pia maisha ya familia kwa kuonjeshana huruma hata katika mambo madogo madogo ya maisha. Mwishoni, anawatakia wote furaha katika huruma kwa kuanzia katika familia zao. Baba Mtakatifu amewapatia heri na baraka wafanyakazi wa Vatican pamoja na familia zao katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.