2015-12-21 09:02:00

Papa apongeza juhudi za kimataifa katika kutatua migogoro, ili kudumisha amani


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 20 Desemba 2015 aliyaelekeza macho na mawazo yake kwenye matukio ya kimataifa huko Syria, Libya, Costa Rica, Nicaragua na India. Baba Mtakatifu anapongeza juhudi za Umoja wa Mataifa zilizochukuliwa kwa ajili ya kukomesha vita huko Syria. Anapenda kuwatia shime wadau wote kuchuchumilia mwelekeo huu ili kusitisha kabisa vita, ili hatimaye kufikia muafaka wa majadiliano na amani.

Baba Mtakatifu pia amewashukuru na kuwapongeza wahusika wakuu katika mgogoro wa Libya waliofikia makubaliano ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kimataifa, ili waweze kujenga matumaini ya Libya iliyo bora zaidi kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu anapenda kuunga mkono juhudi zinazofanywa kwa kuzishirikisha Nicaragua na Costa Rica katika kupata suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizi mbili. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, nchi hizi mbili zitaweza kujenga na kukuza tena udugu kwa kuimarisha majadiliano na ushirikiano pamoja na nchi zote zilizoko kwenye Ukanda huu.

Baba Mtakatifu mwishoni, ameyaelekeza mawazo yake kwa kuwakumbuka na kuwaombea wananchi wa India ambao hivi karibuni wamekumbwa na mafuriko yaliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu ameziweka roho za marehemu wote waliopoteza maisha katika mafuriko hayo chini ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.