2015-12-21 15:26:00

Kanuni msingi katika huduma kwa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam na matashi mema kwa wasaidizi wake wa karibu, “Curia Romana” Jumatatu, tarehe 21 Desemba 2015 amewatakia heri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya amewashukuru wale wote waliohitimisha huduma yao mjini Vatican kutokana na umri pamoja na kuwakumbuka wale wote waliotangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anasema katika kipindi cha miaka mitatu amegusia umuhimu wa kujikita katika weledi na huduma; upatanisho kwa kutaja orodha ya magonjwa yanayoweza kuwakumba wafanyakazi wa Vatican; magonjwa yanayohitaji kinga na tiba, lakini kwa bahati mbaya yameendelea kusababisha kashfa kiasi cha kuleta usumbufu mkubwa katika mioyo ya watu, lakini ikumbukwe kwamba, Kanisa litaendelea kufanya mageuzi katika maisha na utume wake, kwa kujikita katika tija na huduma makini licha ya magonjwa na kashfa kuendelea kujitokeza!

Roho mbaya ni kikwazo cha mageuzi na huduma bora inayotolewa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wale wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika ukweli na uaminifu; wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa kuzingatia weledi na uaminifu; kwa kuonesha faraja, mshikamano, utii na ukarimu wao katika sala. Mapungufu yanayojitokeza miongoni mwa wahudumu wa Vatican ni changamoto ya kurejea tena katika mambo msingi kwa kutambua uwepo wa Mungu na jirani, kwa kuwa na mtazamo wa Kikanisa na Waamini katika ujumla wao.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko ni fursa ya kuonesha moyo wa shukrani, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; upyaisho wa maisha ya kiroho na kiutu pamoja na kujipatanisha na Mungu. Ikumbukwe kwamba, Noeli ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu kwa binadamu; huruma inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kwa mwaka 2015 anapenda kuwashirikisha tunu msingi zinazohitajika kwa wafanayakazi wa karibu na Baba Mtakatifu; kwa wale wote wanaotamani kushuhudia wakfu na huduma makini kwa Kanisa kwa kuambata kwa namna ya pekee huruma, ili kweli iweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha.

Huruma hii inajikita katika umissionari na huduma za kichungaji; kustahili na hekima; tasaufi na utu; mfano bora na uaminifu; fikara na upendo; moyo mkuu na kutowadhuru wengine; upendo na ukweli; heshima na unyenyekevu; Ibada na umakini; ujasiri na utayari; kuaminiwa na kiasi. Haya ndiyo mambo makuu muhimu kwa wale wanaotaka kutoa huduma makini kwa Vatican na Kanisa katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, kila Mkristo ni mmissionari kutokana na dhamana aliyojitwalia wakati wa Ubatizo na kwamba, anatapaswa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Utekelezaji makini wa mikakati ya shughuli za kichungaji ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kipadre, anayetaka kumfuasa na kumuiga Kristo mchungaji mwema. Ni mtu anayejitunza pamoja na kuokoa maisha ya wengine, ili kuonesha kwamba, kweli ni mtumishi mwaminifu.

Mtu akistahilishwa kazi fulani katika maisha anapaswa kuitekeleza kwa ari na kwa umakini mkubwa akitumia akili na busara, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali kwa hekima na busara; kwa kujikita katika haki, wema pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ili mawazo, maneno na matendo yatekelezwe kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Tasaufi ni nguzo muhimu sana katika huduma ndani ya Kanisa na katika maisha ya Mkristo kwa kukabiliana kikamilifu na vishawishi vinavyojitokeza kila siku ya maisha dhidi ya imani. Watu waoneshe utu wao kwa kuguswa na mahangaiko ya wengione, wawe na ujasiri wa kucheka na wale wanaocheka; ujasiri wa kulia na wale wanaoomboleza, tayari kushiriki katika mchakato wa kuleta mabadiliko katika maisha ya watu. Tasaufi na utu na fadhila zinazopaswa kufanyiwa kazi kila siku ya maisha.

Wafanyakazi wa Vatican wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa ili kuepukana na kashfa zinazoweza kudhoofisha uaminifu wa maisha yao kama watu waliowekwa wakfu. Watu wajitahidi kuwa waaminifu hata kwa mambo madogo na anaonya kwamba, ole wake ambaye atakuwa ni sababu ya kashfa ndani ya Kanisa. Watu wajenge utamaduni wa kuwa na fikara na upendo ili kuondokana na ukiritimba usiokuwa na mashiko kwa kuwa na ratiba pamoja na mpango wa kazi unaotekelezeka. Hapa kwa maneno mengine anasema Baba Mtakatifu mtu anakuwa na uwiano bora katika maisha.

Wafanyakazi wa Vatican wanapotekeleza dhamana na majukumu yao wawe na ari na moyo mkuu na kamwe wasiwadhuru wengine. Watende mambo kwa haki huku wakifuata kanuni ya dhahabu na daima kwa ajili ya afya ya roho za watu. Upendo na ukweli ni sawa na chanda na pete; karama zinazokamilishana, ili kuwa wema na makini katika kutenda haki. Uaminifu na ukomavu ni msingi unaoweka uwiano bora kati ya uwezo wa mtu kimaumbile, kisaikolojia na katika maisha ya kiroho; huu ni mchakato endelevu katika maisha ya mwanadamu na kamwe hauna kikomo!

Baba Mtakatifu katika salam zake za Noeli kwa wasaidizi wake wa karibu anakaza kusema, wanapaswa kuonesha heshima na unyenyekevu kwa kuweka kila jambo mahali pake, kwa kutunza siri; kwa kusikiliza kwa makini na kuzungumza kwa heshima na busara, daima wakiomba kufanya yote haya kwa njia ya neema ya Mungu. Waoneshe ibada kwa Mwenyezi Mungu, tayari kutoa na kuwashirikisha wengine kile walichonacho katika maisha!

Waoneshe moyo wa ukarimu na mapendo; uhuru na ukweli bila kujishikamanisha na malimwengu au kuwa na uchu wa mali na madaraka. Watambue mapungufu yao ya kibinadamu na tayari kuyarekebisha. Watu wawe na ujasiri wa kupambana na magumu pamoja na changamoto za maisha bila ya kukata tamaa; kwa kutenda katika uhuru bila kumezwa na malimwengu. Wawe na ujasiri wa kuishi kwa kiasi na kukataa  kujilimbikizia mambo ya dunia, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani.

Mtu mwenye kiasi anatambua namna ya kubana matumizi na kutenda kwa haki. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wasaidizi wake wa karibu kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni, ili kweli huruma hii, iweze kujikita katika mageuzi, maamuzi na utekelezaji wa shughuli mbali mbali zinazofanywa na Kanisa, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huruma ni kashfa kwa haki; ni wazimu kwa wenye akili, lakini faraja kwa wakosefu wanaoishi na kupendwa, wanaoweza kulipa deni lao kwa njia ya huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.