2015-12-21 09:15:00

Juhudi za makusudi zinahitajika kujenga amani Burundi!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss anasema, kuna haja kwa Serikali ya Burundi kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha mara moja mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, na kuanza mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Askofu mkuu Tomasi ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano wa Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili hali ya kisiasa nchini Burundi ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kuvunjika kwa Mkataba wa Arusha wa mwaka 2000 uliohitimisha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi iliyodumu kwa miaka kumi na miwili ni chanzo kikuu cha machafuko ya kisiasa nchini Burundi. Wapinzani wanamtuhumu Rais Pierre Nkurunziza kwa kuvunja mkataba huu kwa makusudi kutokana na uchu wa madaraka, hali ambayo kwa sasa inawatumbukiza wananchi wa Burundi katika machafuko ya kisiasa na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu na kwamba, wananchi wengi wanaendelea kuishi katika hofu na mashaka makubwa kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Tomasi kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaweza kusaidia kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja kukomesha biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hizi ni juhudi zinazopaswa kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa. Wadau mbali mbali nchini Burundi wawe na ujasiri wa kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Wapatanishi wa kimataifa waoneshe utashi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya mwelekeo wa sasa ambao umeshindwa kutoa suluhisho la kudumu huko Burundi na matokeo yake watu wanaendelea kupoteza maisha yao kila kukicha anasema Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi. Burundi haina budi kujikita katika utawala wa sheria na demokrasia ya kweli kwa kuwashirikisha wananchi katika maamuzi mbali mbali sanjari na kuunda mazingira yatakayowahakikishia wananchi amani na usalama wa maisha na mali zao pamoja na kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji kutoka Burundi, wanarejea tena makwao, ili kushiriki katika ujenzi wa nchi yao.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika aliwataka viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao Barani Afrika kusaidia ujenzi wa mchakato wa demokrasia ya kweli inayofumbata mafungamano ya kijamii, maridhiano, heshima, daima kwa kutafuta ustawi na maendeleo ya wengi; mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Uzoefu unaonesha kwamba, mauaji, kinzani na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yanarutubishwa zaidi na woga usiokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu. Watu wanapokata tamaa, wanapoendelea kuelemewa na umaskini pamoja na kuchanganyikiwa, wanaweza kuwa wepesi zaidi kujitumbukiza katika mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.