2015-12-19 16:59:00

Waonjesheni watoto wagonjwa upendo unaosheheni huruma!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa vatican, Jumamosi, tarehe 19 Desemba 2015 ametembelea Hospitali ya Bambino Gesù na kusalimiana na watoto wagonjwa pamoja na wazazi, walezi na wahudumu wa Hospitalini hapo sanjari na kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa watoto hao wagonjwa wakati huu Kanisa linapojiandaa kusherehekea Siku kuu ya Noeli, Kristo anapozaliwa tena katika mioyo na maisha ya watu!

Kardinali Parolin anakaza kusema, Hospitali hii inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ni taasisi nzuri, muhimu na yenye mafao makubwa kwa watoto wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, utume wa wadau mbali mbali ni kuhakikisha kwamba, walau wanawaonjesha watoto hawa huruma inayosheheni upendo.

Akiwa Hospitalini hapo, Kardinali Parolin, amewakilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua kwamba, watoto wagonjwa na maskini wanayo nafasi ya pekee kabisa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Hospitali hii iwe ni mahali pa matumaini na utulivu wa ndani kwa wazazi wanaopeleka watoto wao kupata tiba. Uwepo wake Hospitalini hapo anasema Kardinali Parolin ni sehemu ya utekelezaji wa matendo ya huruma, nilikuwa mgonjwa ukaja kunitazama, changamoto muhimu sana wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu. Matendo haya ni muhimu sana kwa wale wanaoyatekeleza kwani yanawasaidia kugundua ubinadamu wao na kuwa tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Watoto wagonjwa wanapoonjeshwa huruma na mapendo, wanakuwa na matumaini hata katika shida na mahangaiko yao ya ndani!

Kuanzia tarehe 21 Desemba 2015, Uwanja wa Ndege wa Vatican unaanza kutumika kwa ajili ya kutoa huduma ya haraka kwa watoto wagonjwa wanaohitaji tiba maalum. Mama Mariella Enoc anasema kwamba, Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa katibu mkuu wa Vatican wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ametoa msaada wa Euro 150, 000 ili kusaidia uchunguzi wa magonjwa maalum ambayo hadi sasa hayana majina maalum.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.