2015-12-19 14:42:00

Ubruda ni wito mtakatifu unaokabiliwa na changamoto kibao!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema “Ubruda” ni wito mtakatifu ndani ya Kanisa ingawa unakabiliwa na changamoto kubwa ya kutoeleweka na wengi na matokeo yake ni kuonesha ukakasi na kubeza wale waliojisadaka katika maisha haya matakatifu. Ikumbukwe kwamba, huu ni wito halali na mtakatifu kama ilivyo miito mingine yote ndani ya Kanisa, lakini kutokana na historia, mazingira, mitazamo na misimamo ya baadhi ya waamini wito huu umeonekana kuwa mgumu sana pengine hata kuliko miito yote mitakatifu ndani ya Kanisa.

Wito wa Ubruda unadai uangalifu mkubwa katika kuusindikiza na kuuelea ili watawa walei waweze kujisikia kuwa wito wao unapendwa, unaheshimiwa na kuthaminiwa na Mama Kanisa katika ujumla wake. Kihistoria anasema Askofu mkuu Ruwa’ichi kuna watu walioamua kujiunga na maisha haya ya kitawa wakiwa na uamuzi na ukomavu wa maisha, wakajisikia nyumbani kati ya ndugu zao katika Kristo Yesu na wala hawakuwa na mashaka au kupungukiwa chochote katika maisha, wito na utambulisho wao.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anasema, katika historia, ulifika wakati baadhi ya waamini wakaanza kuuangalia wito wa Ubruda katika miwani ya Kipadre. Kwa vijana walioshindwa kufikia wito wa Upadre, basi wakashauriwa kujiunga na Ubruda na tangu wakati huo Ubruda likawa ni chaguo la pili katika maisha ya kitawa na Ubruda ukaonekana kuwa kama ni daraja la mpito! Kwa bahati mbaya, mtazamo kama huu bado unaendelea kujionesha hata miongoni mwa waamini na viongozi ndani ya Kanisa kwani wanadhani kwamba, Mabruda wanapungukiwa na hivyo hawajakamilika katika safari ya wito wao.

Huu ni mtazamo na uelewa tenge kuhusu wito wa Ubruda ndani ya Kanisa. Ulifika wakati katika historia ya maisha na utume wa Kanisa, Mabruda wakaonekana kuwa ni rasilimali muhimu sana katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na ukuaji wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Hawa wakaonekana kuwa ni nguvu kazi isiyokuwa na gharama; nguvu kazi ambayo ingetumika katika ujenzi wa Makanisa na shughuli mbali mbali za ufundi, Mabruda wakatambulikana na wengi kuwa ni wachapakazi kwa bei nafuu!

Kwa masikitiko makubwa Askofu mkuu Ruwa’ichi anakaza kusema, hapa Mabruda walitambulikana kuwa ni wafanyakazi tu, wakaondolewa katika maisha ya kitawa na utambulisho wao ukamezwa. Lakini ikumbukwe kwamba, watawa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wanaotekeleza dhamana na utume wao katika medani mbali mbali za maisha, iwe ni katika ujenzi, huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anapenda kuwapongeza na kuwavulia kofia watawa walei wanaojisikia nyumbani na wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji pamoja na kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda wa huduma ya upendo na vyombo makini vya Uinjilishaji. Lakini kuna baadhi yao hawana uhakika wa maisha, wito na utambulisho wao, hali ambayo inawafanya kutojisikia kuwa huru na nyumbani katika maisha ya kitawa kiasi hata cha kuwa na kigugumizi!

Askofu mkuu Yudda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza anahitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu utambulisho, utume na umuhimu wa waamini walei waliowekwa wakfu kwa kulitaka Kanisa kurejea katika misingi ya Injili na  Mafundisho ya Kanisa kuhusu maisha ya kitawa, ili kuthamini, kuenzi na kuendeleza wito wa maisha ya Mabruda ndani ya Kanisa, wadau muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.