2015-12-19 11:13:00

Ubruda ni wito mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani utakaohitimishwa hapo tarehe 2 Februari, 2016 katika Sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, hivi karibuni limewasilisha Waraka kuhusu “Utambulisho na utume wa mtawa mlei katika Kanisa” kwa kuonesha utajiri na mchango mkubwa unaotolewa na “Mabruda” ndani ya Kanisa mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa wa namna ya pekee kujitaabisha kuusoma ili kusaidia kuhamasisha na kukuza miito ya Ubruda ndani ya Kanisa na Mabruda wenyewe kuendelea kuishi wito huu wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kukutana na  kumwambata Kristo kila siku ya maisha yao! Wito wa Ubruda ni wito mtakatifu na ni sehemu ya maisha ya Kikristo, ambamo watawa walei wanaalikwa kwa namna ya pekee kumuiga Kristo aliyekuwa: Mtii, Fukara na Mseja kamili, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa njia ya huduma makini inayotolewa na Mama Kanisa mintarafu Injili ya Kristo.

Wito wa Mkristo ni kumfuasa Kristo mwenyewe kwa kuchukua sehemu ya utajiri mkubwa unaofumbata maisha ya Yesu na kuanza kuufanyia kazi. Bruda ni mtawa anayemtafakari Kristo katika unyofu wa maisha; wema na utakatifu; kwa kuwa karibu na watu, ili kuwahudumia kwa moyo wa upendo na huruma; anapaswa kuwa ni shuhuda wa ukarimu na mapendo kwa Mungu na jirani; mhudumu wa upendo wa Kristo unaomwilishwa katika huduma mbali mbali.

Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume linakaza kusema, utambulisho na utume wa Bruda unafumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linaloonesha umoja na utofauti; ni zawadi inayoshirikishwa katika maisha ya kijumuiya yanayokumbatia udugu, upendo na mshikamano; zawadi hii ni kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, mahali ambapo watu wote wanajisikia kuwa ni watoto wa Mwenyezi Mungu. Kwa ufupi, mambo haya msingi tayari yalikwishagusiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kichungaji, Maisha ya Wakfu, Vita consecrata n aule uliotolewa na Baraza hili kuhusiana na Ushuhuda wa Utakatifu Mtakatifu, alama ya udugu na huduma ya mapendo.

Baraza la Kiappa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume linawashukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko kwa kuendelea kuhamasisha miito ya kitawa ndani ya Kanisa,  ili kujenga maisha na utume wao kwa kuiga mfano wa Bikira Maria katika huduma; Fumbo la Utakatifu Mtakatifu katika umoja na mshikamano; katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, chemchemi ya maisha na utme wa Kanisa.

Mabruda hawa ni mashuhuda wa huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa  pembezoni mwa jamii. Watawa watambuane kwamba wao wote ni ndugu wamoja, wanaohamasishwa na Mama Kanisa kuliimbia Fumbo la Utatu Mtakatifu, utenzi wa sifa na shukrani, wakiwa wameshikamana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu, wakishuhudia wito na Injili ya furaha wanayoitangaza kwa njia ya maisha na huduma; kwa njia ya Mashauri ya Kiinjili. Watawa wajibidishe kuwa wadumifu katika maisha na wito wao, ili Kanisa liendelee kukua na kupanuka katika huduma na utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.