2015-12-19 09:33:00

Askofu Nkwande: Kumbatieni Injili ya Uhai; epukeni utamaduni wa kifo!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuingia kwenye Lango la huruma ya Mungu kwa ujasiri, huku wakionesha moyo wa toba na wongofu wa ndani; upendo na huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ni muda muafaka wa kuwa na ujasiri ili kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kukimbilia huruma ya Mungu ili kutua mzigo wa dhambi na mapungufu ya binadamu yanayomwelemea mwanadamu.

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha kugundua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha ya waamini, ili kuonja msamaha, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu mambo msingi yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni waamini kukumbatia Injili ya uhai, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Iweni na huruma kama Baba yenu! Ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2016 analenga kuwatuma Wamissionari wa Huruma ya Mungu, watu watakaokuwa na hamasa ya Umama wa Kanisa kwa ajili ya Taifa la Mungu; Mapadre watakaopewa mamlaka ya kuondolea hata dhambi ambazo na Baba Mtakatifu, Maaskofu au Mapadre walioteuliwa kwa nia hii na Maaskofu wao, ili kuwapatia waamini maondoleo ya dhambi zao; Wamissionari hawa wanahamasishwa kuwa waaminifu kwa mambo ya Kimungu.

Askofu Nkwande anakaza kusema, wimbi la utamaduni wa kifo linaendelea kuingia kwa kasi kubwa Barani Afrika, kwa hali ambayo inatisha sana. Haya ndiyo madhara ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu; utandawazi unaokumbatia utamaduni wa kifo. Tatizo la utoaji mimba linaonekana kuwa kama jambo la kawaida kwa watu wengi kwa sasa. Vijana wanapata na kutoa mimba, kuna hata Hospitali na Zahanati ambazo zimebobea katika utoaji mimba, jambo ambalo linakwenda kinyume cha Injili ya uhai anasema Askofu Nkwande.

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uwe ni muda muafaka wa kukimbilia huruma ya Mungu kwa kuachana na tabia ya utoaji mimba, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema sanjari na kuzingatia Mafundisho ya Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Waamini wajenge dhamiri nyofu kwa kuogopa dhambi ya kutoa mimba na badala yake wathamini Injili ya uhai. Utoaji mimba ni mauaji ya kikatili kwa watu wasiokuwa na hatia kama inavyojionesha hata katika vitendo vya kigaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.