2015-12-18 11:58:00

Marehemu Askofu mstaafu Shija alikuwa ni mtu wa imani, matumaini na mapendo!


Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Alhamisi tarehe 17 Desemba 2015 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Askofu mstaafu Mathayo Shija kwenye usingizi wa amani na Ibada ya mazishi imeongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Ibada hii ambayo imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Kahama Tanzania imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Maaskofu pamoja na waamini walei kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Kahama.

Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Padre Alcuin Nyirenda OSB, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Askofu mstaafu Mathayo Shija wa Jimbo Katoliki Kahama; Ibada iliyofanyika kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo, mjini Roma. Kwa namna ya pekee, Padre Nyirenda amewataka Wakleri ambao ni wamissionari wa huruma ya Mungu kumuiga Marehemu Askofu Shija katika imani, matumaini, mapendo na kuwa ni watu wa kiasi katika maisha, daima wakiwa tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu, huku wakichuchumilia utakatifu na maisha ya uzima wa milele, changamoto kubwa inayotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Ndugu zangu, tunaadhimisha Ekaristi Takatifu kwa ajili ya Mhashamu Askofu Mathayo Shija aliyezaliwa mbinguni siku ambayo Tanzania inakumbuka uhuru wa nchi yaani tarehe 9 Desemba 2015. Kadhalika leo ni siku ya kuzaliwa Baba Mtakatifu Francisko. Askofu Mathayo Shija amebahatika kuishi miaka 91 hapa duniani kutoka mwaka 1924 -2015. Ameishi miaka 61 ya upadre toka mwaka 1954 – 2015. Ameishi miaka 32 ya Uaskofu toka 1983–1915. Kutokana na wingi wa miaka aliyoishi na huduma katika wito wake wa Ukristu, Upadre na Uaskofu, kwa vyovyote atakuwa ametenda mambo mengi sana, atakuwa na mang’amuzi makubwa ya maisha tunayoita Hekima, busara na uchaji wa Mungu.

Mimi nimebahatika kuonana naye katika nafasi chache. Nafasi mojawapo ilikuwa ya mikutano ya mabaraza la maaskofu, wakati wa mikutano ya pamoja na wakuu wa mashirika ya watawa. Tulikutana pia kifupi jimboni Kahama akiwa kama askofu mstaafu. Halafu tena alifika monasterini Hanga kwenye sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Askofu Gervas (Frt. Placidus OSB) Nkalanga na jimboni Mbinga. Mang’amuzi niliyopata kila nilipokutana naye yamenifanya nichague masomo haya ili niwazungumzie sifa stahiki za Askofu huyu. Sifa ambazo sisi tunaweza kuziiga kama wanafunzi hasahasa kama wachungaji wa Kanisa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto ya kuwa kweli ni wamissionari wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Masomo niliyochagua ni ya ajabu kidogo hasa ukizingatia mazingira ya leo ya msiba na majonzi. Somo la kwanza ni toka Barua ya kwanza ya Paulo kwa Wakorinto sura ya 13. Sura hii ni Utenzi wa upendo. Kwa kawaida utenzi huu unatumia kwenye misa za ndoa. Katika utenzi huu nimeyapenda hitimisho lake pale Paulo anaposema: “Kwa hiyo, au Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”  Jambo analolikazia Paulo katika utenzi huu ni Upendo. Halafu katikati ya utenzi kuna ubeti mmoja usemao: “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu, na tufananya Unabii kwa sehemu; lakini ijapo (itakapofika) ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabadilika. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.”

Kumbe, kwa njia ya imani tunaweza kumfahamu Mungu, lakini siyo kamili bali kama uakisi wa kioo kwa njia ya uumbaji wake. Kisha tunatumaini kwamba tutaona Mwanga wa Heri  (Mungu) uso kwa uso. Mwanga wa heri ambao“Hakuna jicho lililoona wala sikio lililosikia, mambo yaliyo zaidi ya akili ya mtu, yale ambayo Mungu amewaandalia wale wanaompenda.” Ukifuatilia na kutafakari maisha ya Askofu Shija, unakuta sifa nyingi sana. Ninyi mnazifahamu nyingi zaidi kwa vile mmekaa naye na kufanya kazi pamoja naye. Katika sifa hizo utagundua jinsi maisha na matendo yake yalivyotawaliwa na imani kwa Mungu iliyoongozana na matumaini makubwa ya upendo wa Mungu. Imani ilimsaidia daima kutumaini mwisho mwishoni mwa yote, yaani ile ya kuona waziwazi mafumbo ya mbinguni yaani mwanga wa upendo wa Mungu.

Katika kipindi cha karibu karne moja aliyoishi, ameshuhudia mianzo na miisho ya mambo mengi, kuzaliwa na kufa kwa watu wengi. Ameshuhudia pia jinsi watu wanavyotoa thamani kwa vitu visivyotakiwa kupewa thamani na baadaye mwisho wake unavyosahaulika. Kumbe, imani aliyokuwa nayo juu ya uhalisia wa Mbingu, na matumaini makubwa juu ya huruma na upendo wa Mungu vilimfanya aishi na atende mambo akiangalia mwisho kama wasemavyo wanafalsafa: “Quidquid agis prudenter agas et respice finem” Chochote unachofanya, fanya kwa busara, ukiangalia mwisho.”

Kipengee kimojawapo nilichokiona mimi cha kuishi imani yake akifikiria mwisho (kikomo cha maisha) unaiona katika maisha yake yaliyokuwa ya kawaida kabisa. Mathayo ni Askofu wa pekee niliyewahi kumwona ambaye hakutaka makuu. Nguo zake hazikuwa za kifahari. Hapa ieleweke kuwa kanzu za mapadre sanasana za Maaskofu na Makardinali zinatofautiana kwa gharama kutokana na ubora wa kitambaa. Hata Msalaba na Pete zinatofautiana ubora na gharama. Mavazi ya Askofu huyu yalikuwa ya kawaida na ya gharama ya chini kabisa. Chakula chake kilikuwa cha kawaida. Unaweza kuthibitisha ukweli huu ukimtazama jinsi alivyokuwa mwembamba. Aidha alijichanganya na kjilinganisha na watu wa kila hali hasa wanyonge. Ama kweli alikuwa kama isemavyo kwamba Kuhani ni “ex hominibus pro hominibus” ni yule aliyetwaliwa kati ya watu na kwa ajili ya watu.

Hata baada ya kustahafu kuongoza Jimbo ameendelea kukaa katika nyumba ya kawaida na katika mazingira ya kawaida kati ya watu. Hali hii yamaanisha kwamba Askofu hakuweka moyo na kuthamini ufahari wa duniani hapa na mali yake. Aliwasaidia sana waseminari, mapadre na watu wote bila ubaguzi akitumia vyema mali ya Kanisa. Kama mchungaji alikuwa karibu sana watu akijilinganisha nao hasa kwa maisha ya ufukara na ya kawaida. Tunajifunza kwake kuwa wachungaji wa kawaida, na kuishi maisha ya kawaida kama wanavyoishi watu wa kawaida.

Askofu Mathayo aliishi na kuyafanya hayo yote akimotishwa na upendo wa Mungu. Upendo ambao Mtakatifu Yohane anazungumzia katika barua yake ya kwanza. “Hili ni pendo: si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi” (IYoh. 4:10). Kweli Askofu alijisikia kuwa ni zawadi ya Mungu na akaona amrudishie Mungu shukrani kama alivyosema Mungu “Mpe Kaisari yaliyo yake Kaisari na Mungu yaliyo yake Mungu. Mateo alikuwa zawadi ya Mungu kama linavyomaanisha jina lake Mateo ni zawadi ya Mungu. Mtume Mathayo aliitwa kumfuasa Yesu, akaacha kazi yake ya kutosha ushuru kama TRA ya sasa. Akawa Mtume, akihubiri kwa maneno, na matendo na kwa kuandika Injili. Kadhalika Askofu Mathayo alijijua kama kweli yeye alikuwa ni zawadi ya Mungu naye alikuwa mtoaji zawadi au mfadhili mkubwa kwa wote. 

Waseminari wa jimboni mwake wakati akiwa Askofu walifaidi sana zawadi toka kwa Askofu Mathayo. Akiwaingizia waseminari hao wazo kwamba nao pia ni zawadi ya Mungu na mwito walio nao ni zawadi ya Mungu. Akawahimiza kuishi maisha ya kawaida na kutenda kadiri tunavyoitwa. Tunajifunza kuwa wanyenyekevu katika miito yetu na kuhudumia kwa upendo. Kifupi tunaona katika Askofu Mathayo, imani matumaini na mapendo na kikubwa zaidi ni upendo. Aidha Askofu Mathayo alihubiri sana kwa maneno yake, lakini mahubiri yatakayodumu mioyoni mwetu ni hasa maisha yake mwenyewe.

Injili yetu inahusu sala ya Mwana wa Mungu anayesali kwa Baba yake: “Baba nami naliwajulisha jina lako (yaani kwa wale aliokuwa anawaombea) tena nitawajulisha hilo, ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao nami niwe ndani yao.” (Yoh. 17:26) Upendo wa Mungu uko katika roho za wale waliokuwa mbinguni, wanaofurahia mwanga, amani na heri ya milele, na wanaomwona Mungu uso kwa uso. Sala zetu na Misa hii imsaidie Askofu Mathayo, kuingia mbinguni na kusimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu anayempenda ambaye kutokana na upendo wake alitupenda sisi sote.

Umpe Ee Bwana Raha ya milele na Mwanga wa milele umwangaze! Astarehe kwa amani. Amina.

Na Padre Alcuin Nyirenda. OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.