2015-12-17 11:08:00

Papa Francisko anaadhimisha miaka 79 ya kuzaliwa kwake!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2015 anaadhimisha kumbu kumbu ya kuzaliwa kwake, miaka 79 iliyopita huko Argentina. Ni mtoto wa Mzee Mario Bergoglio na Mama  Regina Sivori ambao hivi karibuni aliwakumbuka katika sala kwa kuadhimisha miaka 80 tangu walipofunga ndoa na huo ukawa ni mwanzo wa ushuhuda wa Injili ya familia iliyokuwa inaundwa na watoto watano, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 17 Desemba 2015 amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia, anapomshukuru na kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa zawadi ya Injili na huduma ya upendo kwa Watu wa Mungu na kwa namna ya pekee kabisa mwanzo mwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Shirika la Don Orione linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kuwashangaza wengi kwa kuonesha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu amekuwa kweli ni chombo cha huruma ya Mungu kwa waja wake.

Wanachama wa Chama cha Michezo Roma, ACLI, wanampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwa kweli mshindi wa huruma ya Mungu na mshikamano na watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, changamoto na mwaliko kwa wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa watu waliokata tamaa katika maisha; kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake barabara, jamii inaweza kusimikwa katika amani na ukarimu, bila kuwatenga watu kwa misingi mbali mbali!

Wanachama wa Benki ya Dawa Italia wanampongeza Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 79 tangu alipozaliwa. Wanamshukuru na kumpongeza kwa kusimama kidete kulinda na kuwatetea wanyonge kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili waweze kupata huduma bora ya afya, kwa kuzingatia na kuheshimu utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hususan, wazee na watoto; ambao wengi wao wanatelekezwa kwa kukumbatia utamaduni wa kifo!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.