2015-12-17 13:53:00

Changamoto za Kanisa kwa sasa: Sinodi, Imani, Sakramenti na Uhuru wa kuabudu


Dhana ya Sinodi, Imani, Sakramenti za Kanisa na Uhuru wa kidini ni kati ya mambo msingi yaliyofanyiwa kazi wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Tume ya Kitaalimungu Kimataifa uliohitimishwa hivi karibuni.Hizi ni mada ambazo zilipendekezwa na wajumbe wa Tume hii ili kuzifanyia kazi na hatimaye kuziandikia Nyaraka maalum. Dhana ya Sinodi kwa nyakati hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anaalikwa kwa na mna ya pekee kabisa kuwa ni chombo cha huduma inayoambata dhana ya Sinodi katika utekelezaji wa sera, mikakati na changamoto za maisha na utume wa Kanisa hasa wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Dhana ya Sinodi ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kielelezo cha umoja na mshikamano katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa. Wataalam hawa wameangalia dhana, historia, taalilimungu na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa katika kukuza na kudumisha urika wa Maaskofu na utekelezaji wake katika ngazi mbali mbali za maisha ya Kanisa bila kubeza taasisi za Kanisa na uwiano wake katika maisha ya kiroho.

Kuna uhusiano wa dhati kabisa kati ya: Imani na Sakramenti; mambo yanayotekelezwa katika mikakati ya shughuli za kichungaji, ingawa hali inatofautiana kutoka katika nchi moja hadi nchi nyingine. Kuna mwelekeo potofu wa kutaka kuondoa imani katika Sakramenti za Kanisa na wengine wanashindwa kuona uhusiano kati ya Sakramenti na Kanisa. Baadhi ya waamini wanataka kupokea Sakramenti za Kanisa hata kama hawana imani, kwani mambo haya yanakuwa ni kama mtindo wa maisha kama inavyotokea kwa baadhi ya waamini kutaka kufunga Ndoa Kanisani hata kama hawana imani na maamuzi magumu wanayofanya.

Wengine wanataka kupata Ibada ya maziko Kanisani hata kama hawana imani katika ufufuko wa wafu na uzima wa milele; mambo yanayofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Mambo yote haya yanaweka mazingira magumu na tatanishi kwa viongozi wa Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kukazia kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya Imani na Sakramenti za Kanisa na kwamba, imani ni muhimu sana katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.

Uhuru wa kidini katika ulimwengu mamboleo ni mada nyingine ambayo imejadiliwa kwa kina na mapana na kwamba, huu ni mwendelezo wa tafakari iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kuhusu utu wa mtu, Dignitatis humanae, miaka hamsini iliyopita. Hadi leo kuna baadhi ya nchi ambamo huru wa kidini bado unadhibitiwa na Serikali dhalimu lakini kwa upande mwingine pia kumeibuka misimamo mikali ya kidini na kiimani; mambo yanayohatarisha utu na heshima ya binadamu. Hapa kuna mwelekeo wa kukosa maana kamili ya demokrasia katika maisha ya watu, hali ambayo inaweza kuhatarisha ustawi na mafao ya wengi. Kadiri ya Mtakatifu Yohane Paulo II, uhuru wa kidini ni msingi wa haki msingi za binadamu na mafao ya wengi; mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na maridhiano kati ya watu ndani ya jamii.

Mada hizi zitaendelea kufanyiwa kazi na Tume ya Kitaalimungu Kimataifa na kwamba,kwa sasa tayari wamekwisha kupata muswada wa tema hizi unaoendelea kufanyiwa tafakari ya kina kwa kuzingatia umoja, udugu na mshikamano unaooneshwa na wajumbe wa Tume hii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wakati wote wa mkutano wao, wameadhimisha kwa pamoja Sakramenti ya Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye mvuto na mashiko wanawaongoza jirani zao kwa Kristo Yesu. Wajumbe hawa wamepata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake siku ya Jumatano mara baada ya kurejea kutoka kwenye hija yake ya kitume Barani Afrika. Tume hii ni chombo muhimu sana kinachomsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa.

Kardinali Gerhard Ludwig Muller, Rais wa Tume ya Kitaalimungu Kimataifa katika mahubiri yake hivi karibuni, amewataka wajumbe wa tume hii kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na ukweli, ili kuzima kiu ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Jukumu lao msingi ni kusoma, kutafakari na kupembua matatizo yanayojitokeza ili hatimaye, kuyapatia ufumbuzi wa kutosha.

Huruma na Ukweli ni mambo muhimu sana wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu. Daima ikumbukwe kwamba, huruma na ukweli ni chanda na pete na kwamba, ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Dhana ya Sinodi katika undani wake ni changamoto ya kumwilisha ushirikiano na upendo, kwa kutembea pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu ambaye ni ukamilifu wa ukweli wote. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Imani na Sakramenti za Kanisa kama njia ya kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, ili waweze kuguswa na huruma na upendo wake unaoganga na kuponya mahangaiko ya mwanadamu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu anakutana na waja wake kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Yesu hamlazimishi mtu kupokea wokovu, bali anamwonesha njia ya kuweza kuufikia wokovu na maisha ya uzima wa milele kwa njia ya imani inayoambata ukweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.