2015-12-17 09:13:00

Burundi inahitaji kuanza mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuambata: huruma, upendo,wongofu, toba na msamaha, tayari kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni nafasi ya pekee sana nchini Burundi ambamo hali inazidi kuwa tete kila kukicha. Bila huruma, msamaha na upatanisho wa kweli, amani haitaweza kupatikana nchini Burundi na matokeo yake, majanga na maafa yataendelea kuwaandama wanchi wengi!

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu Joachim Ntahondereye wa Jimbo Katoliki Muyinga wakati wa uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimboni Muyinga. Akihojiwa na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji anasema, hali ya usalama, amani na utulivu nchini Burundi ni tete sana kutokana na machafuko ya kisiasa na mpasuko wa kijamii unaoendelea kupanuka siku hadi siku baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania madaraka ya Urais kwa awamu ya tatu, kinyume cha Katiba ya Nchi, ambayo kimsingi ni Sheria mama.

Kanisa tangu awali lilipinga hatua hii kwa kuchelea kwamba, ingesababisha mpasuko mkubwa wa kijamii, lakini halikusikilizwa na matokeo yake ni hali ya wasi wasi na mashaka inayoendelea kujionesha kila kukicha nchini Burundi. Kuna mauaji ya kikatili pamoja na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; mambo yanayohatarisha amani nchini Burundi. Maaskofu Katoliki Burundi waliandika barua mbili za kichungaji kwa kuwataka wadau mbali mbali kujenga na kudumisha demokrasia ya kweli, kwa kuwahusisha wote, ili kutafuta mafao ya wengi na haki jamii, lakini hakuna aliyewasikiliza matokeo. Jaribio la kutaka kuipindua Serikali iliyokuwa madarakani, Mwezi Mei, 2015 lilichafua hali ya kisiasa nchini Burundi, kiasi cha vinara wa vyama vya upinzani kulazimika kuikimbia nchi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Lakini hali bado ni tete hakuna usalama wala utulivu.

Machafuko na mpasuko wa kisiasa ni mambo yatakayoendelea pasi na ukomo kwani wengi wanataka kulipizana kisasi. Hapa mwaliko ni kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuanza kwa ujasiri mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Hii ni changamoto kubwa nchini Burundi, ambako Majimbo mbali mbali nchini humo yameadhimisha Sinodi ambazo zimejikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kuna haja ya kushinda kishawishi cha kung’angania vita na kuanza kutafuta suluhu ya haki na amani. Watu waoneshe ujasiri wa kusamehe na kujipatanisha; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kutoa nafasi kwa wakimbizi na wahamiaji kurejea tena nchini mwao, tayari kuendeleza ujenzi wa nchi yao! Kanisa litaendelea kuwekeza zaidi na zaidi katika majiundo makini kwa waamini walei, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wenye mvuto na mashiko! Wanasiasa ambao wengi wao ni waamini wa dini mbali mbali, wanahamasishwa na Kanisa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji wanaojikita katika misingi ya haki na ukweli, daima wakitafuta mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.