2015-12-16 11:45:00

Watawa wanahamasishwa kuwa ni wamissionari wa huruma ya Mungu!


Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, mwaliko kwa watawa kuhakikisha kwamba wanapyaisha maisha yao kwa kumwambata Kristo aliye mwanga, njia, ukweli na uzima. Watawa wawe na ujasiri wa kumuiga Kristo aliyekuwa fukara, mtii na msafi sanjari na kuambata maisha ya kijumuiya, kielelezo cha upendo na mshikamano unaomwilishwa katika mapendo kamili kama wanavyokaza kusema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kardinali Joao Braz de Aviz ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume ulipoanzishwa. Maadhimisho haya yamefanyika wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa namna ya pekee, watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao,  ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayojikita katika huduma makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Neno la Mungu liwe ni daraja linalowaunganisha watawa katika maisha na utume wao kwa kuendelea kujichotea nguvu kutoka katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Watawa wajisikie kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu inayowajibika, tayari kutoka kifua mbele katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya majadiliano ya kina yanayofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Watawa wasijifungie katika ubinafsi wao, bali wawe na ujasiri wa kutoka kifua mbele ili kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kwa namna ya pekee, watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa wamoja katika maisha na utume wao, kwa kujichotea nguvu kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo, lililokuwa linasali na hivyo kujipatia nguvu hata ya kustahimilia kifodini. Katika maadhimisho ya Ibada hii ya Misa Takatifu watawa wanne wametumwa kwenda kusini mwa Italia kusaidia kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha. Itakumbukwa kwamba, Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, linawaunganisha wakuu wa mashirika 1857, wanaotekeleza utume wao sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa wanawaongoza watawa zaidi ya 350, 000.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.