2015-12-16 09:47:00

Jubilei ya watoto katika Mwaka wa Huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Ibada na Sala, Jumapili iyayo, tarehe 20 Desemba 2015, itakuwa ni zamu ya watoto kutoka sehemu mbali mbali za Jimbo kuu la Roma watakaokusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican huku wakiwa wanasindikizwa na wazazi, walezi na Mapadre wao ili kuadhimisha  Jubilei ya huruma ya Mungu pamoja na kushiriki katika Sala ya Malaika wa Bwana, itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mchana!

Hija ya watoto kutoka Jimbo kuu la Roma ni kati ya matukio rasmi ya maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wakati huu, tayari watoto hawa katika kipindi cha Majilio wamejiandaa kwa hali na mali ili kupita kwenye Lango la huruma ya Mungu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Moyo kwa moyo. Wenye huruma kama Baba”. Watoto hawa wameandaliwa vyema ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mtoto Yesu anayezaliwa tena katika maisha yao ya kila siku. Watoto wanaalikwa kwa namna ya pekee, kuiishi furaha ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma kwa kutambua kwamba, wanapendwa na kupokelewa; wanaheshimiwa, wanathaminiwa na kusamehewa na Mwenyezi Mungu wanapokesea. Watoto hawa kutoka sehemu mbali mbali za Jimbo kuu la Roma tangu asuhuhi na mapema watakutanika kuzunguka maeneo ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kushiriki katika tukio hili ambalo kadiri ya Mapokeo ni siku pia ya Baba Mtakatifu kubariki Sanamu za Mtoto Yesu zitakazowekwa kwenye Mapango ya Noeli kwa Mwaka 2015.

Watoto, wazazi na walezi wao, Jumapili ijayo watakuwa ni mahujaji wa huruma ya Mungu Jimbo kuu la Roma. Watatembea kwa furaha, ukakamavu na maringo, huku wakisali na kumwimbia Mungu nyimbo za furaha na shukrani, tayari kukutana na kuambata Huruma ya Mungu katika maisha yao. Watoto hawa watakapowasili, majira ya saa 4:00 za asubuhi kwa saa za Ulaya, wataanza maandamano kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, huku wakipita kwenye Lango la huruma ya Mungu lililofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 8 Desemba 2015. Watoto hawa watashiriki Ibada ya Misa takatifu itakayoongozwa na Kardinali Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, baadaye watakusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali na Baba Mtakatifu ambaye atabariki pia Sanamu za Mtoto Yesu, tayari kuadhimisha Siku kuu ya Noeli ambayo kwa sasa iko mlangoni.

Viongozi wa watoto hawa wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa upendeleo wa pekee katika maisha na utume wake kwa maskini na watoto, mambo yanayowapatia hamasa ya kutekeleza kwa dhati utume miongoni mwa watoto ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Kutokana na mwelekeo huu, viongozi hawa wanataka kuwasaidia watoto kuonja kutoka katika undani mwao ile furaha ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tayari kuwashirikisha pia rafiki na majirani zao waliotawanyika sehemu mbali mbali za Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.