2015-12-15 11:50:00

Mwongozo wa kupambana na ukatili wa majumbani!


Chama cha Wanawake Wakristo nchini Yordani kinasema kimechoshwa na vipigo, nyanyaso na dhuluma inayotendeka katika kuta za familia, kiasi hata cha kuharibu tunu msingi za maisha ya ndoa na famia. Wanawake wanasema, upendo umetoweka na matokeo yake wanaume wengi wanapenda kuonesha ubabe na ukatili wa mfumo dume, mambo ambayo yamepitwa na wakati kwani, mwanamke hapigwi kwa masumbwi wala mateke, bali kwa upande wa kanga! Waathirika wa vitendo hivi ambavyo vinadhalilisha utu na heshima ya wanawake ni walemavu, wasichana na watoto wanaopaswa kulindwa na kuheshimiwa kisheria.

Kutona na changamoto hizi, Chama cha Wanawake Wakristo nchini Yordani, kimeamua kuandika mwongozo wa kupambana na nyanyaso pamoja na ukatili wa majumbani; mwongozo ambao unasindikizwa na kauli mbiu “Utu wangu”. Huu ni mchango mkubwa wa kisheria uliotolewa na wanawake wanaotetea haki msingi za wanawake huko Mashariki ya kati, kwa kuitaka Jamii kuhakikisha kwamba, inaunda vijana wanaofahamu haki na wajibu wao katika jamii, tayari kusimama kidete kuzilinda na kuzitetea kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Mwongozo huu unagusia sheria za kitaifa na kimataifa dhidi ya nyanyaso kwa wanawake majumbani na kwamba, umefika wakati kwa wanawake kutendewa haki zao msingi. Ni sheria zinazokataza ubaguzi wa kijinsia katika maeneo ya kazi au kipato cha mtu! Uzinduzi wa mwongozo huu uliofanyia hivi karibuni umehudhuriwa na watetezi wa haki msingi za wanawake pamoja na watoto wadogo. Kunako mwaka 2008 Yordan ilipitisha sheria ya familia ili kukabiliana na changamoto za uvunjaji wa haki msingi za wanawake na watoto ndani ya jamii.

Takwimu zinaonesha kwamba, wanawake nchini Yordani asilimia 53.8% ya wafanyakazi wote katika sekta ya elimu ni wanawake na wengine asilimia 45% wanawafanya kazi katika sekta ya afya. Kumbe, mchango wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Yordan ni mkubwa, ingawa wananyanyasika sana majumbani mwao, hata kama takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 89.9% ya wanawake waliovuka umri wa miaka kumi na tano, wamekanyaga umande!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.