2015-12-15 07:02:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwanzo mpya wa maisha ya kiroho!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 13 Desemba 2015 amefungua Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, kwa kuwakumbusha waamini kwamba, hiki ni kipindi kikuu cha msamaha. Kwa kufungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Malango yote ya Jubilei sehemu mbali mbali za dunia yalifunguliwa, kwa kuwataka waamini kuwa ni chemchemi ya furaha licha ya shida na magumu yanayowaandama katika maisha kwani Mwenyezi Mungu yuko kati yao!

Kardinali James Michael Harvey, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya kuta za Roma alifungua Lango kuu la huruma ya Mungu kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu matendo ya huruma: kiroho na kimwili; fadhila ambazo zinaendelea kutoweka pole pole katika uso wa dunia. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kama mwanzo mpya katika hija ya maisha yao ya kiroho, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali James Harvey anakaza kusema, Huruma ya Mungu ni Yesu mwenyewe, Msamaria mwema aliyejitaabisha kumganga mwanadamu katika maisha yake ya kiroho kwa kumwondolea dhambi pamoja na kumpatia mahitaji yake msingi. Yesu alihubiri na kushuhudia huruma ya Mungu kati ya watu wake inayopita dhambi na mapungufu ya binadamu, mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao, tayari pia kuwashirikisha wengine. Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kiwe ni kipindi muafaka cha kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na kifani.

Toba inayoambata matumaini ni mwaliko kwa Kanisa zima, ili kuliwezesha kukumbatia mchakato wa kimissionari unaokwenda sanjari na Uinjilishaji mpya, ili waamini waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili. Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda, anasamehe na kuwakirimia waja wake matumaini mapya katika maisha yao. Mwenyezi Mungu anawajia watu wake ili kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti, tayari kuwashirikisha uzima wa milele. Kardinali James Michael Harvey anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, mwanzo huu mpya wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unawezekana ikiwa kama waamini watatambua uwepo na ukaribu endelevu wa Mungu katika maisha, chemchemi ya furaha ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.