2015-12-14 10:42:00

Watawa wote ni ndugu katika Kristo Yesu!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Baada ya kuuzindua Mwaka wa huruma ya Mungu, na kufungua malango ya Jubilei, ambapo kwa namna ya pekee pia tunaalikwa kuyapita malango hayo ya haki ili tuingie na kumtukuza Bwana, huku tukiuacha ukale na kuuambata upya wa moyo na roho, tunaendelea kuienzi huruma ya Mungu ambayo pia inaonekana katika uwepo wa maisha ya kitawa ndani ya Kanisa. Tunakumbushana, tumo pia katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, ambao utahitimishwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016 katika sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni; siku ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II, aliiweka rasmi kuwa ni siku ya kuadhimisha Maisha ya Wakfu.

Hatutasahau kwamba, watawa ndani ya Kanisa, ni watendaji wa huruma ya Mungu. Kwa njia ya maisha yao, sala zao, kazi zao, na mfano wa maisha yao, wao wanaimwilisha Injili ya Kristo kati ya watu. Katika kipindi kile kilichopita tulianza kuona kwa uchache-uchache juu ya historia ya Maisha haya ya kitawa. Pamoja na kwamba kunaweza kuwa na nadharia nyingi; lakini jambo la muhimu ni kwamba, Mkono wa Mungu daima umetenda Makuu ndani ya Kanisa. Mungu daima analishangaza taifa lake kwa jinsi ambavyo anayapamba maisha kwa uwepo wa watu mbalimbali ndani ya Kanisa.

Huu uwepo wa Waamini Walei, Wakleri, Watawa wa Mashirika Mbalimbali na wa Milengo mbalimbali ndani ya Kanisa; tunauona kama ni uzuri wa aina yake, uzuri unaompamba Kanisa, aliye Mchumba wa Kristo. Na hivyo kwa uwepo wa makundi hayo, Kanisa lionaonekana kuwa hai katika uwepo na huduma zake; na pia katika lengo lake, yaani kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili. Tunapoitazama historia ya Maisha ya Utawa watawa na mtindo wao wa maisha, ni vema pia kuona tunaweza kujifunza nini. Maisha hayo yanatuambia nini katika maisha yetu ya kila siku. Kuna tunu nyingi sana za maisha ya kibinadamu, ambazo tunazikuta zimehifadhiwa katika maisha ya kitawa hata nyakati zetu hizi.

Nyakati zile za karne za mwanzo wa Ukristo, Mtakatifu Pakomi aliongokea imani kwa kuangaziwa na jinsi Wakristo walivyowatumikia wafungwa kwa upendo. Mang’amuzi hayo yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo. Na mang’amuzi hayo yaliathiri maisha na mafundisho yake yote. Hivyo baada ya kushika umonaki wa kukaa pweke, akajisikia wito wa kuishi kwa upendo ndani ya jumuiya pamoja na wengine. Hivyo  akaanzisha maisha ya pamoja upwekeni huko kusini mwa Misri. Mtakatifu Pakomi, ndiye wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa, na ndani yake jina ndugu linashika nafasi ya mmonaki. Watawa wakaishi kwa umoja na upendo na wakapokeana kama ndugu. Hivyo maisha ya pamoja yanapata mwelekeo maalumu na kuzaa matunda yanayokusudiwa pale tu, yanapofuata Kanuni maalumu, kwani maisha bila utaratibu, ni uwanja wa fujo.

Ndani ya jumuiya hiyo, waliambata maisha ya mfungo, sala ndefu, kujisadaka kwa ajili ya wengine, kuwa watii  na wenye huruma. Hayo ndiyo maisha ya Upendo aliyoyaagiza Bwana Yesu. Baadaye kidogo, Mtakatifu Basili Mkuu (330-379) naye alianzisha maisha ya pamoja baada ya uona mfano wa Wamonaki sehemu mbalimbali. Naye pia aliita monasteri yake jamaa kwa kuwa lengo lake kuu lilikuwa kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama ilivyokuwa katika lile Kanisa la mwanzo. Tofauti na monasteri ya Mtakatifu Pakomi iliyofikia kuwa na maelfu ya wamonaki, jamaa hiyo haikuwa kubwa sana wala kuwa na ngome, wala kuishi jangwani, bali waliishi karibu na mji wa Kaisarea wa Kapadokia.

Mtakatifu Basili mkuu akiwa Askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa mahalia ili wamonaki wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wafuate utakatifu wa wito wao, tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida; mambo ambayo watawa wanafanya hadi hii leo. Mfumo wake wa maisha ya kimonaki ulizingatia zaidi ushirikiano kati ya ndugu. Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu wamonaki wote wa Mashariki, na kwa njia yao Makanisa ya Kiorthodox kwa vile Maaskofu wao ni wamonaki nao wanaelekeza wakristo wote kufuata mifano yao.

Mpendwa msikilizaji, kwa siku ya leo, kutoka katika mwangwi huo wa Historia ya maisha ya Watawa, tuchote maneno machache, ili yatusindikize nasi katika maisha yetu ya kila siku, nayo ni: Udugu, Umoja, Kanuni/Utaratibu wa maisha na huduma kwa wengine. Sisi pia kama waamini Walei, tunaweza kutumia tunu hizo za maisha ya kitawa ili kuweza kuratibisha maisha yetu ya kila siku. Katika siku zetu hizi ambapo ubinafsi, umimi-mimi na upekepeke unaota sugu hadi kwenye familia, tunu hii ya umoja na upamoja, itusaidie kuzifanya familia zetu na mafungamano yetu kuwa ni maisha ya kijamii zaidi.

Na tukitaka mafanikio, iwe katika maisha ya familia, au maisha ya kazini au katika mafungamano yoyote yale, ni lazima tuongozwe na kanuni maalumu. Familia inayoishi tu bila kanuni yoyote, huwa haikosi chokochoko. Mafungamano yoyote yasiokuwa na kanuni yoyote, huwa ni mwanzo wa fujo zisizokoma na mwisho ni msambaratiko wa wote. Pamoja na kuwa na Imani thabiti kwa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake; kanuni msingi kabisa ni Upendo-Umoja-Uvumilivu na Uwajibikaji katika ukweli.

Mpendwa msikilizaji, hizo ndizo zimekuwa tunu za maisha jamii ya kitawa tangu zamani zile. Hata wewe unaweza ukaziishi hizo, nawe utafurahia mema.Tusikilizane tena kipindi kijacho ambapo tutauangazia Utawa wa Magharibi. Kukuletea makala hii kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Pambo Martin Mkorwe OSB, Mmonaki wa Abasia ya Roho Mtakatifu – Mvimwa Sumbawanga – Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.