2015-12-14 10:13:00

Watanzania wana muuliza Dr. Magufuli na sisi tufanye nini?


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, Jumapili, tarehe 13 Desemba 2015 kwenye Kikanisa cha Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, kanda ya Italia, Roma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu, Tanzania inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 54 ya Uhuru na kazi; mwanzo wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na uchaguzi mkuu kwa Jumuiya ya wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma na kuishi Roma.

 

Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Rugambwa aliyekazia umuhimu wa ujumbe Yohane Mbatizaji na hali halisi ya Tanzania katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki, amani na maendeleo na ustawi kwa watanzania wengi! Dominika ya Tatu ya Majilio ni Dominika ya furaha kwa kuwa Kristo yu karibu. Dominika ya furaha ni tangazo kwa dunia nzima kuwa ukombozi wetu u karibu na mwanzo mpya unakaribia. Ilipokaribia Noel ya kwanza, Mungu alimtuma mjumbe wake; Mtakatifu Yohane Mbatizaji kuandaa ujio wa mwanaye. Yohane anawabatiza watu. Ubatizo wa Yohane ulikuwa kwa ajili ya wongofu na msamaha wa dhambi ili “kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa” (Lk 1:17) na kuandaliwa kwa ubatizo wa Kristo: ubatizo wa Roho Mtakatifu na wa moto.

Sehemu hii ya Injili inaonesha kuwa watu wengi na waliotoka katika makundi mbalimbali ya jamii walifika kwa Yohane kubatizwa. Hata hivyo swali wanalomwuliza Yohane linabaki kuwa swali la msingi: “Tufanye nini basi?” Swali hili linadhihirisha kwamba ubatizo wetu si tendo linaloishia katika ibada bali ni wajibu wa maisha. Jibu la Yohane kwa kila kundi linawaelekeza kutenda haki kwa Mungu na kwa jirani kama sehemu ya wajibu wa kila siku. Huu ni wajibu ambao kila unapotekelezwa, Kristo anakuwa amesogezwa kwa watu. Kwa maneno mengine, sote, bila kujali matabaka yaliyopo, watu wa kawaida, viongozi na watumishi mbali mbali, tunaalikwa kujivika uadilifu, tukitenda haki  ili kuwa wamisionari wa Huruma ya Mungu. 

Tunapojiandalia ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo, tukifurahia uwepo wake kati yetu, tunaalikwa nasi kuwa na mwenendo huo anaoutaja Mtume Paulo katika Barua yake kwa Wafilipi; kuyaweka wazi mahitaji yetu kwake, kwa kusali na kuomba na tukimshukuru kwa mema mengi anayotujalia.     Katika adhimisho la leo tunapenda pia kuunganisha sadaka ya adhimisho hili kwa lengo la kuiombea Nchi yetu inayosherehekea miaka 54 ya uhuru wake. Tunamshukuru Mungu kwa jinsi anavyoendelea kulitunza na kulihifadhi Taifa letu katika amani. Tunamshukuru Mungu pia kwa kuweza kulivusha salama Taifa letu katika kipindi cha uchaguzi uliopita, jambo ambalo linazidi kuonesha jinsi ambavyo Taifa linaweza kukua katika kuiishi mifumo na michakato ya kidemokrasia. Hata hivyo amani ya Taifa letu inapaswa kutafsirika pia katika maendeleo ya watu.

Tunapenda kutumia adhimisho hili kumwombea Rais mpya na Serikali yake. Kwa kipindi hiki cha takribani mwezi mmoja na zaidi, dalili za Tanzania njema zimeanza kujitokeza na kuashiria matumaini makubwa. Kuna kila dalili kwamba Rais John Pombe Magufuli ameazimia kuipitisha nchi kupitia misingi ya uwajibikaji na uadilifu. Yuko anaonesha azma kubwa ya kuziba mianya ya rushwa, ufisadi na urasimu, usimamizi na udhibiti wa rasilimali za nchi na kuirudisha nchi katika misingi ya uadilifu na nidhamu.

Kama wananchi tutamwuliza Rais swali la Injili ya leo: “Tufanye nini basi?” Bila shaka atatuambia kuwa serikali ya awamu ya tano inapenda kulitoa Taifa katika uzembe na rushwa. Onyo la Yohane Mbatizaji la kuwataka watu waache kujinufaisha wenyewe ndiyo msisitizo pia tunaousikia kutoka Tanzania. Bado ni mapema mno lakini tumwombe Mungu ili azma hii ya Rais idumu.

Sisi Watanzania tulio Roma pia tujiulize: “Tufanye nini basi?” Hili ni swali kwa kila mtu. Tunapaswa kujiepusha na kishawishi cha kudhani shida za utendaji mbovu ziko serikalini au zilikuwa ni tatizo la utendaji wa watu wa wakati wa Yohane Mbatizaji tu. Ni tatizo la kijamii na hata ndani ya Kanisa, na kati yetu sisi wenyewe.  Basi tumwombe huyo Yesu Kristo aliyekuja kutuonesha njia na namna ya utendaji, kadiri ya mpango wa Mungu, yeye anayekuja daima na anayependa kukaa nasi, azidi kutuangazia ili tuyafuate na kuyaweka katika matendo, hayo yaliyo tangazwa na Manabii na kwa namna ya pekee, hayo yaliyotangazwa katika ukamilifu na Yeye mwenyewe aliye: Njia, Ukweli na Uzima.  Tusisahau kuwaombea viongozi wa umoja wetu hapa Roma tukiwashukuru wanaomaliza muda wao na kuwaombea mafanikio wale watakaochaguliwa leo kuyachukua majukumu mbali mbali.

Tumsifu Yesu Kristo. 

Wakati huo huo, Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma umechagua viongozi wao na hawa ndio waliopewa dhamana ya kuonesha dira na mwelekeo wa maisha, ili Mungu atukuzwe na mwanadamu aokolewe

1.  Mwenyekiti ni Padre Damian Dotto.

2.  Katibu ni Padre Joseph Msafiri Mahela OSS

3.  Mtunza Hazina ni  Sr. Patricia Amlima OSB

4.  Kiongozi wa Ibada na Liturujia ni Shemasi Felix Luboya.

5.  Mkutubi ni Pd. Peter. Clemence Ndunguru OSS.

 

Na Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.