2015-12-14 11:09:00

Msiomudu kasi ya Magufuli jiwekeni pembeni!


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, amesema wameanza kutumbua majipu madogo katika serikali ya awamu ya tano na kuwaonya watakaoshindwa kwenda na kasi yao wakae pembeni. Akizungumza Jijini Dar es Saalam, mwishoni mwa juma baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Amana, ikiwa ni saa chache tangu atoke Ikulu kuapishwa, alisema katika kuonyesha nia hiyo ndio maana badala ya kwenda kufanya sherehe za kuukwaa uwaziri na ndugu zao waliamua yeye na Waziri wake, Ummy Mwalimu, kwenda Hospitali ya Amana na Mwananyamala kujionea hali halisi ya huduma zinazotolewa.

Kingwangala aliyetembelea kwa kushtukiza Hospitali ya Amana alianza ziara hiyo saa 8:00 mchana na kukuta hali ya utoaji huduma ni mbaya jambo lilomlazimu kutoa maagizo makali kwa uongozi wa hospitali hiyo ikiwemo kukutana nao  Wizarani saa ambapo alidai watapena maagizo ya namna ya kufanya kazi na kwa muda maalum. Alisema muda watakaopena kutimiza jambo fulani kama mtu atashindwa itabidi aondoke apishe wengine watakaoweza kufanya kazi hiyo na kuonya ambao hakuwakuta sehemu ya kazi wameponea chupuchupu kwa kuwa ndio kwanza ameanza na kuonya kung’oa mtu atakapofanya ziara nyingine kama hiyo.

Ziara ilivyokuwa:

Sehemu ya kwanza kutua ilikuwa ni eneo ambalo wagonjwa hupokelewa kabla ya kupatiwa matibabu na kisha kwenda katika vyumba vya madaktari ambapo kati ya vyumba vinne alikuta daktari mmoja huku mwingine akitaarifiwa na wagonjwa waliokuwepo hapo kwamba amekwenda kuosha gari lake. Wakati akipita kote huko hakukuwa na mwenyeji kutoka hospitali hiyo jambo lililomfanya kuzunguka maeneo hayo akiwa na baadhi ya maofisa kutoka Wizara ya Afya. Baada ya kuona hali hiyo alihoji kuwa wenyeji wako wapi na ndipo hapo walipoanza kupigiana simu na baada ya kama dakika 15 akatokea Muuguzi Kiongozi aliyejitambulisha kwa jina la Bupe Mwakagenge, ambaye naye aliendelea kutoa maagizo kusakwa kwa viongozi wa Idara nyingine. Kwingine alipofika ni katika chumba cha x-ray ambacho kilikuwa kimefungwa jambo ambalo alidai halikubaliki kwani kuna wagonjwa wa dharura kama wajawazito na wale wanaopata ajali mbalimbali kutakiwa huduma hizo wakati wowote.

“Jamani kwa ufanyaji kazi kamahuu, chumba cha x-ray ambacho kinatakiwa kufanya kazi saa 24 kimefungwa mchana huu, ni wazi kwamba akija mgonjwa hapa mtamuandikia aende Muhimbili jambo ambalo halikubaliki. Pia alisema kitendo cha uongozi wa hospitali hiyo kuwa na madaktari wawili wa zamu sio sahihi kutokana na wingi wa wagonjwa wanaofika kupata matibabu. Kigwangala alisema malalamiko ambayo ameyapata kwa wananchi waliokuwepo hapo, ni kwamba wamekaa kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi muda huo wa saa 9:00 hawajapata matibabu ni kwa ajili ya uzembe ambao ungeweza kuzuilika. “Haiwezekani daktari mmoja akahudumia wagonjwa wote hawa ninaowaona, na kitaalamu mgonjwa anatakiwa kukaa si zaidi ya nusu kupata matibabu la sivyo ndio maana wengine wanapoteza maisha wakiwa kwenye foleni jambo ambalo hatutalivumilia,”alionya.

Katika chumba cha maabara nako alikuta mashine ya kupimia magonjwa mbalimbali ya Ms50 (fool blood picture), ikiwa imeharibika kwa miezi miwili sasa huku ya Penta8 nayo ikiwa inafanya kazi taratibu na hivyo kuongeza foleni ya watu ambao wamekuwa wakifika kupata huduma katika maabara hiyo. Mmoja wa wazee aliyejitambulisha kwa jina la Amos Litumbu mkazi wa Segerea, alisema alifika juzi na kulipia vipimo wakamwambia aende jana, lakini cha kushangaza tangu alipofika majira ya saa 8:00 usiku hajapata huduma hiyo na kumuomba Waziri amasaidie kwa kuwa mgonjwa aliyempeleka yupo katika hali mbaya.

Mbali na x-ray pia aliingia katika wodi ya wazazi na kushuhudia wakina mama watatu na watoto wao wakiwa wamelazwa kitanda kimoja ambapo alisema ipo haja ya kuongezwa kwa wodi hiyo hata kwa ujenzi wa kwenda juu kwa kuwa suala hilo kiafya halikubaliki. Akilielezea hilo , Muuguzi Kiongozi wa Wagonjwa wa Ndani, Francis Itima, alisema ujenzi wa kwenda juu katika wodi huo umeshindikana kutokana na wahisani waliojenga jengo hilo Benki ya Dunia, kujenga msingi wenye uwezo wa kujenga ghorofa mbili, hivyo wanachofanya ni kutafuta eneo lingine ndani ya hospitali hiyo.

Pia alisema kutokana na changamoto hizo wamekuwa wakijitahidi kuwaruhusu wazazi mara mbili kwa siku pindi wanapojifungua ili kutoa nafasi kwa wengine njia ambayo Kigwangala alikuwa na shaka nayo kwa madai kwamba anachojua mama hutakiwa kupumzika kwa saa 24 baada ya kutoka kujifungua na kutahadharisha kuwa wasiwe wanawaruhusu ovyo ovyo bila kujidhihirisha afya zao. Kwa upande wa duka la dawa la hospitali hiyo, Waziri alishangazwa na kauli ya Mfamasia wa zamu wa hospitali hiyo, Anna Kajiru, kumueleza kwamba kuna jumla ya dawa tofauti 500 wakati kunatakiwa kuwapo kwa dawa 4000 ili kuweza kumpa uhuru mpana daktari wa kumchagulia mgonjwa dawa.

“Hili suala linasikitisha sana , kwa nini duka la dawa la nje liwe na dawa zaidi ya 3000, lakini la ndani lina dawa 400 wakati linahudumiwa watu wengi, naomba suala hili lishughulikiwe haraka sana ,”aliagiza. Wananchi watoa ya moyoni: Baadhi ya wananchi waliokuwepo hospitalini hapo na kufuatilia kila alipoenda Waziri huyo, walitoa malalamiko yao kwamba wauguzi wa Hospitali hiyo wamekuwa na lugha chafu kwao. Joseph Kazizi, Mkazi wa Gongo la Mboto, alisema mbali ya kuwa na lugha chafu wamekuwa wakitumia muda mwingi kuongea na simu na ‘kuchat’ hivyo kupunguza kasi ya kuhudumia wagonjwa.

Kwa upande wa Waziri Ummy Mwalimu, yeye alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Mwananyamala ambako alikutana na malalamiko toka kwa wagonjwa kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo. Akizungumza na wagonjwa mara baada ya kufika Hospitalini hapo jana, wagonjwa walilalamikia kitendo cha watendaji wa Hospitali hiyo, kuwatoza fedha za matibabu hata wale ambao wana msamaha. Salima Omary ni mama wa mtoto Samira Ismail (3) ambaye amelazwa katika wodi za watoto alisema ametozwa Sh. 14,000 kwa kila siku kwa ajili ya matibabu ya mwanaye ambaye aliungua na moto.

Pia Mwalimu alitembelea wodi ya wajawazito na kukuta vyandarua havijafungwa na alipohoji wahudumu wa wodi hiyo walisema vyandarua vipo bali havijafungwa kutokana na wodi hiyo bado haijawekewa sehemu za kufungia. Mmoja wa wahudumu hao katika wodi VB ya wanaume Paul Magembe alisema wanakabiliwa na matatizo ya mashuka, feni na taa nyingine haziwaki. “Wodi yetu ina mashuka 30 huku yanayohitajika yakiwa ni mashuka 60 ili kuweza kubadilisha pale yanapochafuka,” alisema Magembe.

Ummy alisema alichojifunza ni kusikia matatizo ya dawa pale mgonjwa anapopewa vipimo na kuagizwa akanunue huku akishangaa waliopewa misamaha ambao ni watoto na wazee wakilipishwa dawa. “Huduma zinachelewa na haziridhishi tunataka kuzindua namba ya simu siku ya Jumatano wiki hii ili wagonjwa waweze kutoa taarifa kuhusu utoaji huduma Hospitali zote nchini, kazi yangu ni kusimamia utekelezaji wa sera, hivyo nitahakikisha changamoto zote zinatatuliwa katika Hospitali zote,” alisema Mwalimu. Alitoa wito kwa watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa mwongozo na kuzingatia viapo.

Mara baada ya kuongea na wagonjwa, Mwalimu aliikaa kikao na watumishi wa hospitali hiyo kusikiliza kero zao ambapo katika hali ya kushangaza muuguzi wa Hospitali hiyo Hilda Mpondo (58) aliangua kilio na alipohojiwa alisema alianza kazi mwaka 1978 na mafao yake yalikuwa yanaenda NSSF na kudai kuwa mwaka 2015 alipoenda kuangalia mafao yake alikuta milioni mbili na laki moja. Alisema wenzake wenye cheo kama chake LAPF wamefikia milioni 100.

 

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.