2015-12-14 08:24:00

Jumuiya ya Kimataifa ioneshe mshikamano katika utunzaji bora wa mazingira


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 13 Desemba 2015 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aligusia kwa namna ya pekee matukio makuu kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu: mkutano mkuu wa Shirika la Biashara la Umoja wa Mataifa unaoanza Jijini Nairobi tarehe 15 Desemba 2015 kwa kuwahusisha mawaziri wa biashara kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameipongeza Jumuiya ya Kimataifa kwa kufikia makubaliano juu ya udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchini; makubaliano yaliyofikiwa huko Paris, Ufaransa, tarehe 12 Desemba 2015, siku ambayo itakumbukwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuandika historia mpya katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira, nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tukio hili la kihistoria linalopongezwa na wengi, linahitaji kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, yale maamuzi magumu yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Paris yanataekelezwa kwa dhati na wahusika wote bila ubaguzi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa nchi maskini ili ziweze kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira. Yote haya yanawezekana ikiwa kama kanuni auni inayoongoza mchakato wa mshikamano wa kimataifa itazingatiwa.

Jumuiya ya Kimataifa imekubaliana kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, joto la dunia linapaswa kuwa chini ya nyuzi joto mbili sanjari na kuendelea kupunguza hewa ya ukaa inayozalishwa viwandani. Ufaransa iliyokuwa mwenyeji wa mkutano huu imepongeza mkataba huu ambao unachukua nafasi ya Protokali ya Kyoto iliyotiwa sahihi kunako mwaka 1997, lakini hakupata mafanikio yaliyotarajiwa. Marekani katika kipindi cha miaka saba inakuwa ni gwiji la mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Jumuiya ya Kimataifa imekubaliana pamoja na mambo mengine, kuunda mfuko wa hiyari wa kiasi cha Dolla za Kimarekani billioni mia moja kila mwaka ili kuzisaidia nchi maskini duniani kuanza kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira. Wakereketwa wa mazingira wanasema, kiasi hiki cha fedha ni kidogo na kwamba, hakuna nchi ambayo inalazimika kuchangia kisheria, ingawa hii ni hatua kubwa katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira, nyumba ya wote.

Mkataba wa utunzaji bora wa mazingira utaisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana na umaskini; kuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na amani. Huu ni mwanzo wa safari ndefu inayojikita katika uwajibikaji wa utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Paris si tu kwa maneno, bali kwa njia ya vitendo. Ni changamoto ya kuendelea kutunza mazingira, nyumba ya wote. Hapa kunahitajika utashi wa kisiasa na mshikamano wa dhati kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.