2015-12-14 08:49:00

Iweni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini!


Kardinali Berhaneyesus Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa, Ethiopia, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anawaalika waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni mafuta ya huruma na mapendo, kwa wote wanaoteseka na kusumbuka: kiroho na kimwili. Kardinali Sourahiel ameyasema haya wakati wa kuzindua maadhimisho ya Mwaka mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Lideta Maria.

Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu maana ya huruma ya Mungu, tayari kuimwilisha kama ushuhuda wa imani tendaji kwa jirani zao. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuonja ndani mwao huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho kwa ajili ya maondoleo ya dhambi.

Lakini kwanza kabisa, waamini wanapaswa kutambua kwamba, ni wadhambi na wanahitaji huruma na upendo wa Mungu. Wakiisha kuipokea huruma hii, wawe wepesi pia kuwamegea na kuwagawia jirani zao huruma ya Mungu pale wanapotindikiwa kutokana na sababu za kibinadamu. Mwenyezi Mungu amemsamehe binadamu dhambi zake kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo na kumjalia maisha ya uzima wa milele. Waamini katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu wajitahidi kujipatia neema na rehema zinazotolewa na Mama Kanisa kwa kutimiza masharti yaliyowekwa, yaani toba na wongofu wa ndani, kupokea Sakramenti na kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu.

Waamini watakapokuwa wanapita kwenye Lango la huruma ya Mungu, wawe na ujasiri wa kuuvua utu wa kale uliochakaa kama kiatu cha raba, tayari kumwambata Kristo Yesu na kutembea katika mwanga na mapito yake! Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamezinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015 na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Jubilei ya huruma ya Mungu itahitimishwa hapo tarehe 20 Novemba 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Kutokana na umuhimu wa waamini kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, Makanisa mahalia yametenga Makanisa maalum ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili waweze kujichotea huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na matendo ya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.