2015-12-14 09:13:00

Iwe ni fursa ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya majadiliano


Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga, wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake Barani Afrika, amewatembelea kama mjumbe na shuhuda wa amani, changamoto kwa waamini na wananchi wote wenye mapenzi mema nchini Afrika ya kati kuambata mchakato wa haki, amani na maridhiano, ili utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi yaweze kupewa msukumo wa pekee katika sera na mikakati ya kisiasa, kijamii na kidini nchini humo.

Kitendo cha Mahakama kuu ya Kikatiba Afrika ya Kati kuondoa jina la aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Bwana Francois Bozize kutowania nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo mwishoni mwa mwaka 2015, kilizua tafrani miongoni mwa wananchi wanaomuuga mkono. Askofu Nzapalainga ametembelea ngome ya PK5 kwa miguu na kuwataka wananchi wa sehemu hiyo kubomoa kuta za utengano unaojikita katika udini na ukabila usiokuwa na mashiko, tayari kuambata mchakato wa haki, msamaha na upatanisho wa kitaifa; tayari kusamehe na kupokea msamaha kutoka kwa wengine, tayari kuonjeshana huruma ya Mungu iliyoletwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao na kujionesha kwa namna ya pekee katika uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Safari ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Afrika ya Kati iliwagusa wengi kiasi cha kusikika wakisema, tunataka amani na wala si vita tena. Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea eneo ambalo wengi waliliona kuwa ni la hatari kwa usalama na maisha ya Baba Mtakatifu, lakini akaonesha ule ujasiri wa imani, upendo na udugu unaovunja kuta za utengano, ili wote kujisikia kuwa ni watoto wa Baba mmoja, na kwamba, tofauti zao za kiimani kisiwe ni kikwazo cha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu! Vijana wa Kiislam na Kikristo wameweka chini silaha zao, tayari kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili amani iweze kutawala katika akili na mioyo yao, tayari kuitolea ushuhuda wa kweli.

Hivi karibuni, Askofu mkuu Luis Mariano Montemayor, Balozi wa Vatican nchini Senegal, Cape Verde, Guinea Bissau na Mauritania, katika mahubiri yake kwa wahamiaji na wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Zongo alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kujikita katika: upendo, msamaha na huruma ya Mungu; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Iwe ni fursa kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha kwa ujasiri kama alivyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa nchini Afrika ya Kati. Watu wanataka kuona mabadiliko yanayowapatia matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Wanachi wengi wana imani, lakini mipasuko ya kidini na kisiasa inatokana na masilahi ya watu wachache wanaotaka kuendelea kufaidika na vurugu hizi kwa mafao yao binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.