2015-12-13 10:11:00

Yaliyojiri kwenye mkutano wa Makardinali Washauri wa Papa Francisko


Baraza la Makardinali washauri wa Baba Mtakatifu Francisko, limehitimisha mkutano wake wa kumi na mbili ulioanza tangu tarehe 10 – 12 Desemba 2015 na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu mwenyewe. Baraza jipya la Kipapa la Walei, familia na maisha pamoja na Baraza la haki, amani na wahamiaji ni kati ya mambo makuu yaliyojadiliwa na Makardinali hawa wakati wa mkutano wao. Haya yamebainishwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 12 Desemba 2015.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki alipata nafasi ya kuwashirikisha Makardinali washauri, dhamana, utume na changamoto ya Baraza hili katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Imekuwa ni nafasi pia ya kusikiliza kwa undani dhana ya “Sinodi” na umuhimu wake kwa Kanisa Katoliki katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, dhana ambayo inaonekana kuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi.

Hii ni sehemu ya mageuzi yanayopaniwa na Baba Mtakatifu kwa Kanisa ili kugawana na kushirikishana maamuzi mazito katika maisha na utume wa Kanisa badala ya maamuzi haya kufanywa na mtu mmoja peke yake! Tema hii itapembuliwa kwa kina na mapana katika mkutano utakaofanyika mwaka 2016 ili kutoa mwelekeo wake mintarafu uelewa wa Kanisa na ufafanuzi wa kitaalimungu. Mada hii imechambuliwa na Kardinali Christoph Schonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria. Baraza la Kipapa la Walei, familia na maisha limejadiliwa na kukamilishwa, Makardinali wamemwachia dhamana Baba Mtakatifu Francisko kuyafanyia maamuzi hayo waliyojadiliana. Baraza la Kipapa la haki, amani na wahamiaji limekamilika na tayari litaweza kutolewa maamuzi na Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Lombardi anaendelea kusema kwamba, Makardinali wamepata pia nafasi ya kusikiliza taarifa ya mageuzi yanayofanywa na Baraza la Uchumi la Vatican kuhusiana na masuala ya fedha, uchumi na uongozi, kama ilivyowasilishwa na Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Baraza hili la Kipapa pamoja na taarifa kutoka kwa Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Uchumi Vatican. Wameonesha mageuzi yaliyokwisha kufanyika na matokeo yake hadi sasa. Mchakato wa mabadiliko katika masuala ya fedha, uchumi na uongozi yanaendelea kufanyiwa kazi ili kukuza ukweli, uwazi, uwajibikaji na tija. Ili kufanikisha malengo haya, Kardinali Pell ameunda tume ya watu wachache watakaopembua kuhusu mwelekeo wa uchumi wa Vatican kwa siku za usoni kwa kuangalia mapato na matumizi ya Vatican. Tume hii itawashirikisha wawakilishi kutoka katika taasisi mbali mbali za Vatican. Makardinali wamepongeza mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana hadi wakati huu na kuwataka wakuu wake kuendelea kufanya mageuzi kwa ari na moyo mkuu pasi na wasi wasi.

Kwa upande wake, Kardinali Sean O’Malley ameshirikisha kazi ya Tume ya Kipapa kwa ajili ya kuwalinda na kuwatetea watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia pamoja na uundwaji wa kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia masuala maalum kama vile programu za elimu, majiundo na huduma ya msaada kwa Mabaraza ya Maaskofu, ili kuwa na mwongozo elekezi kwa ajili ya Makanisa mahalia. Mwishoni, Baraza la Makardinali washauri kwa kushirikiana na Baba Mtakatifu Francisko wameamua kwamba, watakutana tena kuanzia tarehe 6 hadi 9 Februari 2016 baadaye, tarehe 11 hadi 13 Aprili 2016; tarehe 6 hadi tarehe 8 Juni 2016; tarehe 12- 14 Septemba 2016 na hatimaye, tarehe 12 hadi tarehe 14 Desemba 2016.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.