2015-12-13 10:49:00

Papa aunda Tume maalum ya kushughulikia sekta ya afya!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza kwa kina na mapana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ameamua kuanzisha Tume ya Kipapa itakayoshughulikia Sekta ya afya ili kuwasaidia viongozi wa Kanisa wanaoshughulikia sekta ya afya kuongeza tija na ufanisi, pamoja na kuendelea kuzingatia karama ya waanzilishi wa Mashirika yao hadi pale itakapoonekana kwamba, kunahitajika mabadiliko kwa kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu Francisko amempatia Kardinali Parolin, dhamana ya kuanzisha Tume maalum ya Kipapa kwa ajili ya huduma katika sekta ya afya kwa viongozi wa Kanisa wenye dhamana kisheria.  Kardinali Parolin, tayari amekwisha chapisha sheria na kanuni zitakazoongoza Tume maalum kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Vatican. Tume hii itakuwa na Rais atakayesaidiwa na wajumbe sita wataalam katika masuala ya huduma ya afya, uongozi, rasilimali, fedha na uchumi. Tume hii itasaidiwa na Katibu mkuu na itakuwa madarakani kadiri ya sheria na kanuni za Vatican.

Tume hii itawajibika moja kwa moja kwa Katibu mkuu wa Vatican na itaweza kutekeleza wajibu wake katika masuala ya: sheria na fedha. Tume hii itashirikiana pia na Baraza la Kipapa la huduma ya kichungaji katika sekta ya afya na inaweza pia kuwashirikisha wataalam, washauri au mashirika mbali mbali. Tume hii itakuwa na wajibu wa kufanya upembuzi wa jumla kuhusu muundo endelevu wa sekta ya afya inayotolewa na Kanisa kisheria, ili hatimaye, kuwa na mbinu mkakati wa muda mrefu sanjari na mahusiano ya Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Tume pia itawajibika kutoa ushauri na suluhu ya matatizo na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya afya kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali iliyopo inatumika vyema kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa kwa ajili ya mafao ya jamii husika. Watakuwa na wajibu wa kusoma alama za nyakati ili kuwasaidia viongozi wa Kanisa kumwilisha karama ya Shirika mintarafu mazingira ya wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.