2015-12-13 11:03:00

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Mexico: 12-18 Februari 2016


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe ametangaza kwamba,  kuanzia tarehe 12- 18 Februari 2016 anatarajia kwenda nchini Mexico kwa ajili ya hija yake ya kitume na kwamba, tarehe 13 Februari 2016 anatarajia kutoa heshima zake za dhati kwa Bikira Maria kwenye Madhabahu ya Guadalupe pamoja na kumkabidhi Bikira Maria mahangaiko, matatizo, furaha na matumaini ya wananchi wa Amerika ya Kusini.

Akiwa nchini Mexico, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na: Viongozi wa Serikali, Wanasiasa na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Mexico. Baba Mtakatifu katika mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu atakutana na familia ya Mungu nchini Mexico ili kuadhimisha kwa pamoja Mafumbo ya Kanisa kwa kukazia zaidi matendo ya huruma kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na ulimwengu wa wasomi kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kitamaduni yanayopania kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Mexico, atakutana na familia, ili kuzihamasisha kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai, tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadri ya mapenzi ya Mungu. Hii ni changamoto na kuondokana na utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu atakutana na Wakleri na Watawa; Wanovisi na Majandokasisi, ambao anapenda wawe kweli ni mihimi biora ya Uinjilishaji unaofumbata huruma na upendo wa Mungu kwa kutambua kwamba, wao ni wagawaji wakuu wa huruma ya Mungu kwa watu wanaowahudumia. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, vijana ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wao. Akiwa nchini Mexico atabahatika pia kukutana na vijana ili kuwatie shime kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji kati ya vijana wenzao katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu atakutana pia na ulimwengu wa wafanyakazi ili kukazia umuhimu wa kazi na ajira; haki msingi za wafanyakazi pamoja na wajibu wao kwa Jamii husika. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kurejea mjini Vatican jioni tarehe 17 Februari 2016 na kuwasili majira ya jioni kwa saa za Ulaya, hapo tarehe 18 Februari 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.