2015-12-13 11:49:00

Endelezeni hija ya toba na wongofu wa ndani kwa kuambata haki na mshikamano


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kufungua Lango la huruma ya Mungu na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laternano, Jumapili tarehe 13 Februari 2015 alirejea tena mjini Vatican ili kusali Sala ya Malaika wa Bwana na waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu anasema, ujumbe wa Yohane Mbatizaji kwa makundi mbali mbali yaliyomwendea ulijikita kwa namna ya pekee katika hija ya toba na wongofu wa ndani unaombata haki, mshikamano na kiasi; mambo yaliyopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu.

Toba na wongofu wa ndani ni muhimu ili kuweza kuambata wokovu unaoletwa na Yesu Kristo kwani Mwenyezi Mungu anataka watu wote waweze kuokoka kwa kukumbatia huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa kutoa na kupokea msamaha wa kweli unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu anakaza kusema haya ni mambo msingi katika hija ya maisha ya Wakristo hapa duniani, ili kuweza kupata furaha ya kweli. Inahitajika imani thabiti ili kuzungumzia furaha katika maisha ya mwanadamu wa nyakati hizi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, mwanadamu anaandamwa na shida, magumu na changamoto zinazomnyima ile furaha ya kweli. Lakini ikumbukwe kwamba, furaha ni sehemu ya vinasaba vya Wakristo kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko karibu nao katika shida na mahangaiko yao ya kila siku. Bikira Maria awasaidie waamini kuimarisha imani yao, ili kuweza kumpokea na kumkaribisha Mwenyezi Mungu chemchemi ya furaha anayetaka kukaa kati ya watu wake.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza macho yake kwenye mkutano mkuu wa biashara kimataifa utakaofanyika huko Nairobi, Kenya kuanzia Jumanne tarehe 15 Desemba 2015 kwa kuhudhuriwa na Mawaziri wa biashara, ili waweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kusikiliza na kujibu matumaini ya wananchi wanaotoka katika nchi zinazoendelea; watu wenye kiu ya maendeleo ya kweli pamoja na kuzingatia mafao ya familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ufunguzi wa malango ya huruma ya Mungu kwenye Makanisa mahalia uwe ni changamoto kwa waamini kuambata huruma ya Mungu kwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma hii. Malango ya huruma ya Mungu yatafunguliwa hata katika maeneo maskini na yenye vita na kinzani. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kutuma salam na matashi mema kwa wafungwa wote duniani, lakini kwa namna ya pekee wafungwa kutoka Gereza la Padua waliokuwa wameunganika na Baba Mtakatifu kwa njia ya sala. Anawashukuru kwa kutumbuiza kwa njia ya muziki. Baba Mtakatifu pia anawashukuru wadau mbali mbali wa Zahanati ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini kwa ushuhuda, mshikamano na ukarimu kwa watoto wagonjwa pamoja na wazazi wao. Amekazia majadiliano ya kidini yanayojikita katika ushuhuda wa maisha ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.