2015-12-12 09:44:00

Yesu Kristo hakimu mwenye huruma!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Desemba 2015 ametia sahihi kwenye Hati mpya inayojulikana kwa lugha ya Kitaalam “Rescritto ex audentia” inayoshughulikia mchakato wa utenguzi wa ndoa zenye utata na hatimaye kuchapishwa na Vatican tarehe 11 Desemba 2015. Hati hii imeanza kutekelezwa wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kufuatia nia binafsi ya Baba Mtakatifu aliyoitangaza kwenye Hati ya Yesu Kristo Hakimu mwenye huruma ijulikanayo kama “Mitis Iudex Dominus Iesus” na ile ya “Huruma katika hukumu” “Mitis et Misericors Iesus” iliyochapishwa kunako tarehe 15 Agosti 2015 wakati wa Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba,  wanatekeleza dhamana na wajibu wao wa kichungaji katika masuala ya ndoa kwa kuzingatia msingi ya haki na huruma kwa wanandoa wanaoendelea kuishi katika hali ngumu ya maisha ya ndoa na familia na kwamba, ndoa hizi ziko hatarini kutenguka. Hati hii mpya inataka kuweka uhusiano mwema kati ya mageuzi mapya yaliyoletwa na Baba Mtakatifu Francisko sanjari na kuzingatia kanuni na sheria zinazotumika na Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki, wakati huu ambapo inasubiri pia marekebisho ya baadhi ya sheria zake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mababa wa Sinodi ya Familia iliyohitimishwa hivi karibuni wamelitaka Kanisa kuwa karibu sana na watoto wake wanaoogelea katika unyonge kutokana na upendo wa maisha yao ya ndoa na familia kutikishwa kwa majeraha makubwa kiasi hata cha kutoweka kabisa. Kanisa linapenda kuonesha ukaribu wake kwa familia hizi, ili ziweze kuonja kazi ya tiba na uponyaji unaofanywa na Kristo Yesu kwa njia ya miundo mbinu ya Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, taasisi hizi zitasimamiwa na kuendeshwa na Wamissionari wa huruma ya Mungu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taasisi ya familia.

Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini dhamana na wajibu wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki “Rota Romana” ndani ya Kanisa sanjari na kulinda umoja  na majiundo makini kwa watumishi wa Mahakama za Kanisa. Utaratibu mpya unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu ambao umegawanyika katika vipengele sita, hautoi mwanya kwa waamini kukata rufaa ikiwa kama wamefunga ndoa kadiri ya sheria za Kanisa.  Dekano wa Mahakama kuu ya Rufaa anayo madaraka kisheria kuweka kando Sheria zinazohusu mchakato wa kutengua ndoa. Hakutakuwa na gharama inayotozwa na Mahakama kuu ya Rufaa, isipokuwa pale waamini wenyewe watakapoona inafaa kimaadili, ili kuwasaidia wanandoa maskini kupata haki yao msingi. Sheria hizi mpya zinafuta sheria zote ambazo zimetangulia ambazo zinakinzana na sheria hii ya marekebisho ya mchakato wa kutengua ndoa zenye utata.

Kwa upande wake, Pio Vito Pinto, Dekano wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki anakaza kusema, Marekebisho ya mchakato wa utenguaji wa ndoa zenye utata yanaonesha mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko unaotaka kujibu kilio cha Mababa wa Sinodi ya Familia kuhusu waamini wanaoishi katika ndoa tata kwa kutambua kwamba, Kanisa linaundwa na wadhambi wanaotaka kutubu na kumwongokea Mungu pamoja na watakatifu wanaoishi kadiri ya neema wanazokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Jumuiya ya waamini inajitambua kwamba inaundwa na wadhambi wanaotaka kukimbilia toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuwa watu wapya wanaojikita katika huruma ya Mungu.

Sheria iliyokwisha kupitishwa na hatimaye kufanyiwa marekebisho tena na Baba Mtakatifu kwa sasa inafunga mjadala wa majadiliano na kwamba, inapaswa kutekelezwa kama inavyotakiwa, ingawa inaweza kukabiliana na changamoto katika utekelezaji wake. Lakini ikumbukwe kwamba, sheria za Kanisa ni kwa ajili ya afya ya roho za waamini ambazo Khalifa wa Mtakatifu Petro ni mwalimu na mhudumu wake wa kwanza! Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki inatekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia hekima na wasi wasi wa jumla, lakini Mahakama ndogo zinaweza kuonesha wasi wasi maalum. Hapa Mahakama zinapaswa kutambua kwamba, ni mhudumu wa Kanisa katika haki na utakatifu wa maisha. Waamini wanayo haki ya kupokea tamko la haki bila malipo, kwani ni sehemu ya haki yenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.