2015-12-12 07:35:00

Waluteri na Wakatoliki shikamaneni ili kumshuhudia Kristo Yesu!


Katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita, Mababa wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican walitoa changamoto kubwa kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anaendesha majadiliao ya kiekumene ili kuwawezesha waamini kushirikiana kwa pamoja, tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu. Majadiliano ya kiekumene yamekuwa yakitekelezwa katika ngazi za kitaifa na kimataifa na matunda yake yanaanza kuonekana sehemu mbali mbali za dunia.

Hivi karibuni, Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Marekani na Waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Marekani wametia sahihi kwenye Tamko la pamoja linaloonesha dira na mwongozo  wa kufuata katika: Kanisa, Utume na Ekaristi Takatifu. Mambo haya ni muhimu sana katika mchakato wa kuelekea kwenye umoja unaoonekana miongoni mwa Wakristo wa Makanisa haya mawili. Hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 tangu Martin Luther alipoanzisha mageuzi makubwa kunako mwaka 1517 na huo ukawa ni mwanzo wa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Marekani alikazia kwa namna ya pekee umuhmu kwa Wakristo kuendeleza majadiliano ya kiekumene yanyojikita katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa waamini wa dini nyingine. Viongozi wa Makanisa haya mawili wanakaza kusema, hiki ni kielelezo cha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayopania kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Wakristo nchini Marekani.

Viongozi hawa wanasema, miaka mia tano iliyopita, ilisheheni kinzani, migogoro na vita ya silaha na maneno, kiasi cha kubakiza magumu na machungu katika maisha ya Wakristo. Leo hii kurasa hizi chungu za maisha na historia ya Kanisa zimepitwa na wakati, sasa wanasonga mbele katika umoja, upendo, mshikamano na ushuhuda wa pamoja kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa miaka mingi, Daraja Takatifu la Upadre na Ekaristi Takatifu vimekuwa ni chanzo kikuu cha mgawanyiko na mitafaruku ya kiimani.

Kuna mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo ikilinganishwa na mambo machache yanayoendelea kuwagawanya. Hii ni changamoto ya kutaka kuendeleza majadiliano ya kiekumene katika masuala ya kichungaji na kitaalimungu, ili siku moja Wakatoliki na Waluteri waweze kuwa wamoja katika Kristo Yesu, mchungaji mkuu wa Kanisa lake. Haya ndiyo matumaini yanayobebwa katika tamko la pamoja kati ya Wakatoliki na Waluteri huko Marekani, mambo yatakayoendelea kufanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani pamoja na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani linalounganisha Jumuiya za Kikristo 145 kutoka katika nchi 98.

Viongozi wa Makanisa haya mawili wanasema, kuna haja ya kuanza mchakato wa majadiliano mintarafu mambo ambayo kwa sasa yamewekwa kando, ili kuweza kufikia umoja kamili wa wafuasi wa Kristo. Pamoja na mambo mengine, viongozi hawa wanataka waamini wa Makanisa haya mawili, kujitahidi kuondoa vikwazo vya kitaalimungu, ili waweze kushiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi takatifu, yaani Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo, alama muhimu sana katika majadilino ya kiekumene.

Wakatoliki na Waluteri tangu mwaka 2011 wameendelea kuhimiza umoja na ushirikiano miongoni mwa waamini katika Makanisa mahalia, tayari kushuhudia upendo wa Mungu unaojikita katika huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni changamoto ambayo imewahi kutolewa pia na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo, mambo ambayo yamepewa msukumo wa pekee katika Hati ya waamini wa Kanisa Katoliki na Waamini wa Kanisa la Kiluteri nchini Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.