2015-12-12 08:32:00

Umoja wa Mataifa waipongeza Vatican kwa kusimama kidete dhidi ya ubaguzi


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss anasema, Umoja wa Mataifa unaipongeza Vatican kwa juhudi zake katika utekelezaji wa malengo ya Umoja wa Mataifa yanayopania kutokomeza aina zote za ubaguzi. Umoja wa Mataifa umempongeza pia Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kupinga umaskini wa hali na kipato kwa kuwatetea na kuwahudumia maskini, ili kulinda utu na heshima yao. Mara nyingi maskini ni kundi linalobaguliwa na wengi kwa misingi ya kidini, kikabila au rangi ya mtu.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anakaza kusema, Umoja wa Mataifa pia umepokea kwa mikono miwili upembuzi yakinifu uliofanywa na Vatican katika mapambano dhidi ya ubaguzi sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, mkazo wa pekee ni kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu vinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kuwahamasisha watu kujikita katika mchakato wa majadiliano, upatanisho na heshima; mambo ambayo yanatiliwa mkazo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mchakato huu pia unafumbata mshikamano na ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi, hasa wale wanaotoka Mashariki ya Kati, kwani wengi wao wananyanyasika na kubaguliwa kwa misingi ya udini usiokuwa na mashiko wala mvuto!

Vatican inapongezwa pia kwa kutunga sheria ambazo inatoa adhabu kwa watu wanaohusika na vitendo vya ubaguzi katika eneo lake. Itakumbukwa kwamba, Vatican ni kati ya nchi 177 zilizoweka sahihi katika Mkataba wa Kimataifa unaopinga vitendo vya kibaguzi. Vatican pia imetoa mapendekezo kadhaa yanayopaswa kufanyiwa kazi, ili kweli Mkataba huu wa kimataifa uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Waathirika wa vitendo vya kibaguzi kwa misingi ya kidini, rangi au mahali anapotoka mtu, wanapaswa kupewa fidia pale ambapo vitendo vya ubaguzi vimefanywa dhidi yao.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema, Umoja wa Mataifa unaendelea kuipongeza Vatican kwa kuwashirikisha watu mbali mbali katika miundo mbinu ya utawala wake, jambo ambalo linaonesha mwelekeo wa Kanisa la kiulimwengu linalofumbata Familia ya binadamu bila ubaguzi. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu. Takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya watoto na vijana millioni 64 wanapata huduma ya elimu kwenye taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Kanisa lina miliki na kutoa huduma katika hospitali 5, 000 ambazo zinawahudumia watu mbali mbali, wengi wao wakiwa ni maskini wanaotoka pembezoni mwa jamii. Wote hawa wanahudumiwa kwa misingi ya kiutu na wala hakuna ubaguzi wowote kwani huduma makini kwa familia ya binadamu ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Hata hivyo Kanisa Katoliki limeshutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda kunako mwaka 1994. Kwa viongozi wa Kanisa wanaotuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda wanapaswa kufikishwa kwenye mkondo wa sheria ili haki iweze kutendeka. Suala la usawa wa kijinsia anasema Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi halikupewa msukumo wa pekee katika vikao vya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswiss. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa makini ili kudhibiti vitendo vyote vya ubaguzi vinavyoweza kujitokeza kutokana na misimamo ya baadhi ya maisha ya watu ndani ya jamii, bali kila mtu anapaswa kuheshimiwa pamoja na kuzingatia kanuni maadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.