2015-12-12 14:41:00

Askofu mkuu Vito Rallo ateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Morocco


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Vito Rallo kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Morocco. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Vito Rallo alizaliwa kunako tarehe 30 Mei 1953 huko Mazara del Vallo, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 1 Aprili 1979 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. Tarehe 12 Juni 2007 akateuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Burkina Faso. Akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu hapo tarehe 28 Oktoba 2007. Katika utume wake kama Balozi, amewahi pia kuiwakilisha Vatican nchini Niger.

Wakati huo huo, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amemteua Padre Fabrizio Meroni kuwa Katibu mkuu mpya wa Shirikisho la Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa Kimataifa, PMU, nafasi ambayo hapo awali ilikuwa inatekelezwa na Padre Vito del Prete ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Shirika la Habari za Kimissionari, Fides. Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa alimtambulisha Padre Meroni kwa wafanyakazi wengine hapo tarehe 7 Desemba 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.