2015-12-11 14:39:00

Papa asikitishwa na vifo vya Makardinali wawili!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na vifo vya Makardinali wawili: Julio Terrazas Sandoval, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Santa Cruz de la Sierra, Bolivia pamoja na Kardinali Carlo Furno, Mhudumu mkuu mstaafu wa Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Makardinali wote wawili wamefariki dunia tarehe 9 Desemba 2015.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambi rambi kwa familia ya Mungu nchini Bolivia anapenda kuungana nao kwa njia ya sala wakati huu wanapoomboleza kifo cha Kardinali Sandoval, ili Mwenyezi Mungu aweze kumjalia amani mtumishi wake ambaye kwa njia ya mwanga wa imani pamoja na nguvu ya matumaini, amekuwa mwaminifu katika utume wake kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Injili, haki na amani. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, wakati huu wa majonzi na masikitiko makubwa, Kanisa linaendelea pia kujiandaa kwa ajili ya kusherehekea Fumbo la Umwilisho, chemchemi ya matumaini. Baba Mtakatifu anawaweka waombolezaji wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume wote wanaoshiriki katika msiba huu mzito. Mazishi ya Kardinali Sandoval yanafanyika nchini  Bolivia, Ijumaa tarehe 11 Desemba 2015.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kutokana na kifo cha Kardinali Carlo Furno. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa huduma na mchango makini uliotolewa na Marehemu Kardinali Carlo Furno enzi ya uhai wake kama Balozi wa Vatican katika nchi mbali mbali na hatimaye, kama Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na Kiongozi mkuu wa Shirika la ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalemu. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na wale wote wanaoomboleza kutokana na msiba huu mzito na anamwombea Marehemu Kardinali Furno usingizi wa amani, huku akisindikizwa na Bikira Maria, afya ya Warumi. Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia baraka zake, wote walioguswa kwa msiba huu mzito!

Habari zaidi kutoka Vatican zinasema kwamba, Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Ijumaa jioni, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Carlo Furno kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko aliwaongoza waombolezaji katika Ibada ya mazishi. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka Jimbo kuu la Roma. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.