2015-12-11 14:48:00

Huruma na upendo ni vinasaba vya maisha ya ndoa na familia


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, baada ya kutembelea kwenye kambi ya wakimbizi na wahamiaji nchini Ugiriki, ameguswa kwa namna ya pekee kabisa namahangaiko ya watu wanaoteseka, wanaonyanyasika na kudharauliwa, wakati wanapojitahidi kusalimisha maisha yao kutokana na hali ngumu ya maisha inayowasibu katika nchi zao.

Anaishukuru Caritas Internationalis inayoshirikiana bega kwa bega na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Ugiriki, Caritas Ellass kutoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji huko Idomeni, mpaka kati ya Ugiriki na Macedonia. Watu hawa wameacha yote nyuma yao na mioyoni mwao wanabeba familia zao, kito cha thamani kilichobakia katika maisha yao kwa sasa. Licha ya matatizo na mahangaiko ambayo watoto wanakabiliana nayo, bado wanaweza kuonja upendo na faraja kutoka kwa wazazi wao.

Mababa wa Sinodi ya familia wameguswa sana na mahangaiko, madonda na kinzani zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa familia. Talaka, “Vidumu” au “nyumba ndogo” ni chanzo cha mahangaiko makubwa kwa familia na kielelezo cha kukosekana kwa uaminifu dhamana ambayo Baba Mtakatifu anawaalika wanandoa kuitunza kama mboni ya jicho, ili amani, upendo na ustawi viendelee kutawala katika maisha yao. Umaskini na hali ngumu ya uchumi ni mambo yanayopelekea baadhi ya familia kuvunjika na wanaoteseka zaidi ni watoto na wanawake wanaojikuta wakihudumia familia peke yao.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu na familia wakati wa raha, wakati wa shida na hasa zaidi wakati wa mahangaiko na mitikisiko ya kiimani. Viongozi hawa waziangalie familia kwa jicho la huruma na upendo kama alivyofanya yule Msamaria mwema aliyeguswa na mahangaiko ya jirani yake, kiasi cha kushuka na kuanza kumhudumia. Familia zinapaswa kuhudumiana na kusaidiana kwa hali na mali, huku zikiongozwa n ana jicho la Kristo mchungaji mwema.

Familia zishirikishane: furaha, matumaini na magumu ya maisha, ili kweli ziweze kuwa ni mashuhuda amini wa Injili ya familia ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kanisa. Familia zionje uwepo endelevu wa Mungu anayewaumba, akawapenda na kuwakomboa kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kardinali Tagle anakaza kusema, maadhimisho ya Sinodi ya Familia ni tukio endelevu ambalo litaendelea kufumbatwa na kukamilishwa vyema zaidi wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ha huruma ya Mungu. Hapa Mama Kanisa anapaswa kuunganisha kwa namna ya pekee: Huruma ya Mungu, haki na mapendo; tunu ambazo Baba Mtakatifu Francisko anazipatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, mwaliko kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, zinamwilisha pia tunu hizi katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Waamini waonje huruma ya Mungu inayokamilishwa katika haki na upendo; mambo yanayokwenda pamoja. Haki ya kweli inapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya huruma kwa wote.

Kardinali Tagle anakiri kwamba katika maisha na utume wake, amebahatika kuhudhuria na kushiriki katika Sinodi sita za Maaskofu na kila Sinodi imekuwa na mafanikio pamoja na changamoto zake zinazojitokeza kutokana na utofauti wa tamaduni, lugha  na jamii ya watu. Lakini wote wanaunganishwa na kifungu cha: Imani, Mapokeo ya Kanisa, Neno la Mungu pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, daima Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza katika yote!

Umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, ndoa tenge na magonjwa ya muda mrefu ni kati ya changamoto kubwa ambazo Kanisa pia linapaswa kuzivalia njuga katika maisha na utume wake, kwa kuendelea kuwa aminifu kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kuitangazia Familia ya Mungu Injili ya matumaini licha ya magumu wanayokabliana nayo. Familia maskini kwa sehemu kubwa zimekuwa ni chemchemi ya matumaini na uaminifu; familia zinazodhani kwamba, zimebahatika kuwa na utajiri, mara nyingi humo pia Shetani amejenga makazi yake! Hizi ni familia zenye litania ya matatizo na machungu anasikitika kusema Kardinali  Luis Antonio Tagle, ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.