2015-12-10 08:19:00

Vatican inawapongeza wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu kwa huduma!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss anashiriki mkutano mkuu wa thelathini na mbili wa Chama cha Msalaba Mwekundu Kimataifa kwa kutambua mchango wa chama hiki katika kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa njia ya mshikamano wa dhati hususan katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola ulioibuka huko Magharibi mwa Afrika na kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu.

Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu walijisadaka ili kuhakikisha kwamba, wagonjwa wa Ebola wanahudumiwa kwa heshima na pale walipofariki dunia, wakazikwa kama binadamu. Kanisa Katoliki nalo limetoa mchango mkubwa katika kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kitaifa na kimataifa. Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anapenda kutoa tuzo maalum kwa wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa Ebola pamoja na kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zinazoongoza Chama cha Msalaba Mwekundu katika utoaji wa huduma kwa waathirika wa majanga mbali mbali.

Hapa kuna haja ya kuendelea kuimarisha sheria za kimataifa kuhusu huduma za kiutu, ili ziweze kutekelezwa na wadau mbali mbali. Kanuni ya kwanza inayopaswa kupewa uzito wa pekee ni kusimama kidete kulinda maisha ya binadamu kwa njia ya huduma bora ya afya pamoja na kuheshimu utu wake. Lengo ni kukuza na kudumisha urafiki, ushirikiano na amani ya kudumu miongoni mwa jamii ya kimataifa. Changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa zinapaswa kufanyiwa kazi inayoonekana na wala si maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa. Mapambano dhidi ya umaskini hayana budi kuendelezwa kwani umaskini unawanyima watu wengi haki zao msingi.

Ujumbe wa Vatican unapenda kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inayapatia ufumbuzi wa kudumu maeneo yote ambayo kwa sasa yamegubikwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, tayari kusimama kidete kuzuia vita na kinzani za namna hii kutokea tena kwa kujikita katika sheria za kimataifa, ili kupunguza athari za kinzani hizi kwa maisha ya watu na mali zao. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuonesha utashi wa kisiasa, kuwekeza zaidi katika ukuaji wa uchumi pamoja na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sera makini inayoweza kuzuia kwa kiasi kikubwa athari zote hizi ni kwa njia ya maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuboresha hali kwa kupunguza gharama ya maisha; kwa kusimamia haki msingi za binadamu na uhuru bila kuwasahau wala kuwatenga maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utawala bora na utawala wa sheria ni nyenzo muhimu katika ustawi na maendeleo ya wengi. Kushindwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza sheria na kanuni msingi kumesababisha maafa kuendelea kusambaa sehemu mbali mbali za dunia, jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusitisha vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Watu wajenge utandawazi wa mshikamano kwa kuguswa na mahangaiko ya jirani zao. Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kupambana na rushwa, vita na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Familia ya binadamu inahimizwa kujenga umoja na mshikamano wa kidugu ili kuendeleza mafao ya wengi.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa inakabiliwa na hofu ya ongezeko la matumizi ya silaha; wimbi kubwa la wahamiaji, umaskini, vita na magonjwa ya kutisha; mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu; yanatishia maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Haya ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuwa na dunia iliyo bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.