2015-12-10 09:34:00

Moneyval yaipongeza Vatican kwa kudhibiti utakatishaji wa fedha chafu!


Mkutano mkuu wa Kamati ya Wataalam wa shughuli za udhibiti dhidi ya  utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili kwa vitendo vya kigaidi, kwa kifupi Moneyval kutoka Jumuiya ya Ulaya, umepitisha kwa kauli moja taarifa kutoka Vatican kuhusiana na sera pamoja na mikakati inayoendelea kuchukuliwa dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi.

Kwa mara ya kwanza taarifa kama hii ilitolewa kunako mwaka 2012, taarifa ya pili ikachapishwa kunako mwaka 2013 katika kikao cha kawaida cha Moneyval. Thathmini hii inafanywa kwa kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya. Moneyval imeridhishwa na hatua mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na Vatican katika kupambana na tatizo la utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili kwa vitendo vya kigaidi.

Moneyval inaitaka Vatican kuendelea kuimarisha miundo mbinu ya fedha, sheria na utekelezaji wake ili kudhibiti kabisa utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi. Vatican kwa sasa inaendelea kufanya marekebisho makubwa katika mfumo wake wa fedha, sheria na kanuni ili kupambana na uhalifu na makosa ya jinai yanayotokana na utakatishaji wa fedha haramu anasema Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, wakati akiongoza ujumbe wa Vatican kwenye mkutano mkuu wa Moneyval hivi karibuni huko Strasburg.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.