2015-12-10 15:42:00

Mhamasishaji wa miito, Kardinali Sandoval amefariki dunia!


Kardinali Julio Terrazas Sandoval, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Santa Cruz de la Sierra, Bolivia, amefariki dunia tarehe 9 Desemba 2015 akiwa na umri wa miaka 79. Marehemu Kardinali Sandoval alizaliwa kunako mwaka 1936. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapewa Daraja takatifu la Upadre hapo tarehe 29 Julai 1962. Kunako tarehe 15 Aprili 1978 akateuliwa kuwa  Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Santa Cruz de la Sierra, Bolivia na kuwekwa wakfu kuwa Askofu 8 Juni 1978.

Kunako mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Oruro na kukabidhiwa madaraka hapo tarehe 25 Machi 1982. Kwa miaka mingi alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia. Mwaka 1991 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santa Cruz de la Sierra, Bolivia. Wakati wa uhai wake, alijitaabisha kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kiasi cha kujenga Seminari mpya Jimbo mwake. Kunako mwaka 2001 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali. Akang’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 23 Mei 2013. Alikuwa ni mjumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.