2015-12-09 16:34:00

Dr. Magufuli amewakuna watanzania! Yaani we acha tu!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema zoezi la usafi lililofanyika leo nchini kote lisiishie hapo bali liwe endelevu ili Tanzania iwe na taswira nzuri kwa wageni wanaoingia nchini.Ametoa wito huo Jumatano, Desemba 9, 2015 kwenye soko la Kariakoo wakati akishiriki zoezi la kufanya usafi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutaka maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru yasiwepo na badala yake watu wote washiriki kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amewataka viongozi wa soko la Kariakoo wafike ofisini kwake Jumatatu ijayo Desemba 14, 2015, saa 4 asubuhi ili wamueleze wana mikakati gani ya kuboresha utoaji huduma kwenye soko hilo. "Natambua kuwa siyo sahihi kupanga chini biashara tulizonazo. Nataka hawa viongozi waje wanieleze wana mpango gani endelevu wa kuboresha soko hili," alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa. Waziri Mkuu ambaye alienda kufanya usafi kwenye soko hilo, alilazimika kuzungumza na mamia ya wananchi waliofika kushiriki zoezi hilo. Pia alikagua maeneo mbalimbali ya soko hilo hadi shimoni na kusema aneridhika na usafi uliofanyika bali amesisitiza usafi huo uendelezwe.

"Kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais Magufuli ya HAPA KAZI TU inatupa ari ya kufanya kazi. Fanyeni kazi. Watanzania mko huru kufanya kazi yoyote lakini cha msingi fuateni taratibu na kanuni. Serikali hii tumamua kuwajali watu wa chini. Tutahakikisha wajasiriamali wadogo, akinamama lishe na wamachinga mnafanya kazi kwa amani na utulivu, " alisema. Rais Magufuli aliamua kuitangaza siku ya Desemba 9, 2015 ambayo ni maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru iwe ni siku ya kufanya usafi nchi nzima ili kuepukana na magonjwa mbalimbali na hasa kipindupindu.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.