2015-12-09 08:09:00

Bikira Maria Mama wa Huruma ya Mungu, Utuombee!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili iliyoko kwenye Uwanja wa Spagna, Jumanne jioni tarehe 8 Desemba 2015 alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko Roma, ili kutoa heshima yake kwa Bikira Maria afya ya watu wa Roma, “Salus Popoli Romani” pamoja na kuyaweka maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu alipowasili Kanisa hapo alikutana na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema waliompokea kwa makofi na vigelegele. Amesali kwa kitambo kidogo na baadaye akasalimiana na waamini waliokuwa nje ya Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kurejea tena mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016, tarehe Mosi Januari anatarajiwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, ili watu waweze kumwendea Kristo tayari kujipatanisha naye kwa kuambata maisha mapya yanayojikita katika upendo na huruma.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Uso wa huruma, Misericordiae vultus anakaza kusema, Bikira Maria alibahatika kufahamu kwa kina Fumbo la Upendo wa Mungu kwa njia ya Huruma iliyofanyika mwili, Bikira Maria akawa mtu wa kwanza kuingia katika Hekalu la huruma ya kimungu kwa kushiriki kikamilifu Fumbo la upendo wake. Bikira Maria ni sanduku la Agano lililohifadhi huruma ya Mungu, hata Huruma hii ikawa ni faraja kwa watu wengi wanaopitia Lango hili.

Bikira Maria alikuwa ni shuhuda wa kwanza wa huruma ya Mungu alipokuwa amesimama pale chini ya Msalaba. Hii ni huruma inayowakumbatia wote pasi na ubaguzi, mwaliko kwa waamini kumkimbilia Bikira Maria ili aweze kuwaangalia kwa jicho lenye huruma, huku bondeni kwenye machozi; waamini wawe tayari kushangazwa na Huruma ya Mungu. Kutokana na Ibada kwa Bikira Maria, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki amekua daima akikimbilia maombezi, tunza na huruma kutoka kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Hii ni safari ya ishirini na tisa kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.