2015-12-09 07:52:00

Askofu Ngalalekumtwa: Iweni na huruma!


Iweni na huruma kama Baba Yenu wa mbinguni ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliozinduliwa tarehe 8 Desemba 2015 na Baba Mtakatifu Francisko kwa Ibada ya Misa Takatifu sanjari na ufunguzi wa Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu Frahncisko katika Waraka wake wa kitume kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwamba katika huruma, waamini wanapata uthibitisho wa upendo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuwashirikisha wengine wanaohitaji huruma na upendo.

Kwa maneno mengine, waamini  na watu wote wenye mapenzi mema wanaalika na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha yao, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu uwe ni mwaka wa kuganga na kuponya majeraha ya utengano kwa njia ya mafungamano, umoja na mshikamano; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; tayari kusikiliza na kujibu kilio cha mateso na mahangaiko yao ya ndani.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania  katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu Tanzania inapoadhimisha kumbu kumbu ya uhuru wake sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawataka waamini na watanzania wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mvumilivu, msamehevu na mwenye huruma na mapendo kwa wote. Sifa hizi za Mungu ziwawezesha watu kuambata fadhila hizi katika maisha yao ili kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Askofu Ngalalekumtwa anawataka watanzania kuiga sura na mfano wa Baba mwenye huruma, ili waweze kuwa wakamilifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni. Huruma ni neno la msingi linaloashiria kazi ya Mungu katika uumbaji, ukombozi na utakatifu; mambo yanayofumbata upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo. Wakristo wanaitwa kuambata huruma katika hija ya maisha yao ya kila siku. Huruma ni msingi thati wa maisha na utume wake kati ya watu wa mataifa.

Ukuu wa Kanisa unajionesha katika huruma na mapendo, mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wanadamu wa nyakati hizi, ambao wanaonekana kusahau kwa haraka uwepo wa huruma ya Mungu ambayo ni kiini cha historia nzima ya wokovu. Mwenyezi Mungu anamfundisha mwanadamu kutumainia wokovu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalohitimishwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Pasaka ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. 

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika waamini na watanzania wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wanaoneshana upendo, haki, amani, huruma, msamaha na upatanisho wa kweli kwani katika safari ya maisha, vitimbwi kamwe havikosekani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.