2015-12-08 09:22:00

Papa Francisko azindua maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko amezindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watu ambao wako tayari kuuvua utu wao wa kale na kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kiroho. Ibada hii ya Misa Takatifu imekwenda sanjari na maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili pamoja na ufunguzi wa lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kupitia lango la Jubilei ya huruma ya Mungu mintarafu mwanga wa Neno la Mungu, ili kuambata rehema na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria alipopashwa habari juu ya Fumbo la Umwilisho. Bikira Maria alialikwa kwa namna ya pekee kufurahi kutokana na upendeleo mkubwa aliokuwa amepewa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni Mama wa Mungu, Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Ujumbe huu unakuwa ni chemchemi ya furaha na imani inayoruhusu neema ya Mungu kuleta mabadiliko katika mioyo ya watu, tayari kuleta mabadiliko makubwa katika historia ya binadamu! Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili inaonesha kwa namna ya pekee ukuu wa upendo wa Mungu unaosamehe dhambi; unaomkinga mwanadamu na madoa ya dhambi na kumhakikishia wokovu! Dhambi ya kwanza iliyotendwa na Adam na Hawa inafutwa kwa mradi wa Mungu unaojikita katika upendo. Mwanadamu daima anakabiliwa na kishawishi cha kutotii kwa kutaka kutenda kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu. Hii ndiyo changamoto inayomwandama mwanadamu kila siku ya maisha yake kiasi hata cha kuvuruga mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Uwepo wa dhambi duniani unaweza kufahamika anasema Baba Mtakatifu Francisko mintarafu mwanga wa upendo wa Mungu unao samehe kiasi cha kumkirimia mwanadamu ahadi ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa njia ya Kristo Yesu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu Baba. Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili ni ushuhuda wa utekelezaji wa ahadi ya Mungu dhidi ya dhambi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni zawadi ya neema ya Mungu, changamoto kwa waamini kugundua ndani mwao huruma ya Mungu kwa kuikumbatia katika hija ya maisha ya mtu binafsi. Ni kipindi cha kukua na kukomaa katika uelewa wa huruma ya Mungu, msamaha na maondoleo ya dhambi. Hata wakati wa hukumu ya mwisho, Mwenyezi Mungu atahukumu kwa kipimo cha huruma. Waamini wanapopita kwenye Lango la huruma ya Mungu wajisikie kwamba, wanashiriki katika upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuondokana na wasi wasi na woga usiokuwa na mashiko wala mvuto, ili kuambata upendo wa Mungu ili kumwilisha furaha ya kukutana na neema inayoleta mabadiliko ya ndani. Kwa kuvuka Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa mara nyingine tena tanaadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha Mtaguso huo tukio ambalo ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican umeliwezesha Kanisa kuwa na Nyaraka muhimu sana zilizoliwezesha Kanisa kuanza hija ya kukutana na watu wa nyakati hizi, kielelezo cha uwepo na nguvu ya Roho Mtakatifu anayelihamasisha Kanisa kutoka kifua mbele tayari kuambata ari na mwamko wa kimissionari, ili kukutana na watu katika medani mbali mbali za maisha. Huko anasema Baba Mtakatifu ndiko ambako Kanisa linatumwa kuwatangazia watu Injili ya furaha. Huu ndio mwaliko unaotolewa na Kanisa hata kwa nyakati hizi kwa kuwataka waamini kuwa na ari na mwelekeo mpya wa kimissionari. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni changamoto makini ya kuambata roho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuwa ni Wasamaria wema kama alivyokaza kusema Mwenyeheri Paulo VI wakati anahitimisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini kwa kupitia Lango la huruma ya Mungu wawe tayari kuwa kweli ni Wasamaria wenye huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.