2015-12-08 15:44:00

Kanuni maadili, mafao ya wengi na mshikamano ni muhimu sana kwa Cop21


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika hotuba yake kwa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa kimataifa juu ya udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa, Jumanne tarehe 8 Desemba 2015 anasema, sera na mikakati inayoibuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu inaonesha moyo mkuu na ujasiri wa kutaka Jumuiya ya Kimataifa kufikia muafaka unaojikita katika kanuni maadili pamoja na kuwashirikisha watu wengi kwa ajili ya mafao na ustawi wa familia ya binadamu inayoambata mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni!

Kardinali Turkson ameyasema hayo wakati huu ambapo Jumuiya ya Kimataifa inaendelea na mkutano wake kuhusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa mchango wa Kanisa unaojikita katika mafao ya wengi yanayoiambata familia yote ya mwanadamu. Anasema, hakuna mtu mwenye haki ya kuharibu mazingira na pale yanapoharibiwa, waathirika wakuu ni maskini na akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi!

Kumbe, kutokana na mwelekeo huu, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuendelea kufumbia macho dhuluma na ukosefu wa haki na usawa unaojitokeza kutokana na uharibufu mkubwa wa mazingira, kiasi cha kuwatumbukiza baadhi ya watu katika majanga na umaskini wa hali na kipato. Hakuna mtu mwenye haki ya kukipokonya kizazi kijacho uwezekano wa kuishi maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote anakaza kusema uharibu mkubwa mazingira ni matokeo ya sera na mikakati tenge ya uchumi na maendeleo, mambo ambayo yanapaswa kurekebishwa kwa kuibua mikakati ya sera za maendeleo zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu, utunzaji bora wa mazingira na maendeleo endelevu yanayozingatia teknolojia rafiki.

Hapa kuna haja ya kuwa na wongofu wa kiekolojia kwa kuibua teknolojia rafiki badala ya kuendelea kutumia nishati ambayo imekuwa ikizalisha kwa kiasi kikubwa hewa ya ukaa ambayo kwa sasa inahataraisha ustawi na maendeleo ya binadamu. Kardinali Turkson anakaza kusema, kanuni maadili, mafao ya wengi sanjari na mshikamano ni mambo muhimu sana katika utekelezaji wa sera na mikakati inayopania kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia. Ukosefu wa kanuni maadili kimekuwa ni kizingiti katika majadiliano yanayoendelea kwenye mkutano huu mjini Paris, Ufaransa.

Mataifa ambayo yamechangia katika uchafuzi mkubwa wa mazingira yanapaswa kuchangia pia kwa kiasi kikubwa ili kuzisaidia nchi changa duniani kuwa na teknolojia rafiki na mazingira. Ni matumaini ya Kardinali Turkson kwamba, makubaliano ya mwisho yatakatofikiwa huko Paris yatazingatia kwa namna ya pekee utashi wa kisiasa, ujasiri na utekelezaji unaowajibisha kisheria kwa watu wote bila ubaguzi. 

Mkutano kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kimataifa unapaswa kuwa endelevu kwani kiasi cha dolla trillioni mbili zinahitajika kila mwaka. Kiasi hiki ni sawa na pato ghafi la taifa kwa mataifa mwengi duniani sawa na matumizi ya kijeshi kwa baadhi ya nchi. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha moyo wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukuza na kulinda utu na heshima ya binadamu; kuzuia na kukinga majanga, kinzani na vita, ili hatimaye kujenga msingi wa haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Viongozi wa kimataifa watambue kwamba, binadamu wote wanaunda familia moja ya binadamu, kumbe wanapaswa kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.