2015-12-08 10:56:00

Hata familia zinapaswa kuonjeshana huruma ya Mungu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss katika mkutano wake wa mwaka ulihitimishwa hivi karibuni, pamoja na mambo mengine wamegusia maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Sinodi hii ilikuwa na inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Maaskofu wanasema familia inapaswa kujikita katika fadhila ya huruma, ili iweze kuwa ni chombo cha huruma na mapendo kwa jirani, kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji.  Upatanisho katika ukweli na haki; huruma na msamaha ni nyenzo muhimu sana katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kusshuhudia Injili ya familia. Serikali inayo wajibu mkubwa wa kulinda na kuzienendeleza familia, ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Maaskofu wanawapongeza Wabunge wanaoendelea kukazia ndoa thabiti kati ya bwana na bibi kama kielelezo cha mwendelezo wa mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu kwa kukataa kishawishi cha kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo! 

Bado kuna nyanyaso za kijinsia zinazofanyika kwenye familia, kumbe hapa pia kuna haja ya kuonesha moyo wa toba, wongofu wa ndani, huruma na msamaha wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Watu wawe na ujasiri wa kuondokana na matendo maovu, tayari kuanza mchakato wa utakatifu wa maisha kwa kukumbatia huruma ya Mungu katika maisha yao.

Maaskofu katika mkutano huu, wameonesha pia mshikamano wao wa dhati na wakimbizi pamoja na wahamiaji kutoka Mashariki ya kati, ambao wengi wao ni watoto na wanawake wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha. Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kuwaonjesha watu hawa upendo na ukarimu, kielelezo cha imani tendaji. Sadaka itakayokusanywa Makanisani wakati wa Siku kuu ya Noeli, itatolewa kusaidia kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.