2015-12-07 09:24:00

Utunzaji bora wa mazingira unakwenda sanjari na mapambano dhidi ya umaskini


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 6 Desemba 2015 amesema kwamba, anafuatilia kwa umakini mkubwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi unaoendelea huko Paris, Ufaransa. Anapenda kuwauliza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa swali msingi ambalo ameuliza katika Waraka wake wa kichungaji juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si, Je, ni dunia ya namna gani ambayo wanataka kuwarithisha watoto wao watakaofuatia baadaye?

Kwa ajili ya mafao ya nyumba ya wote, kila mtu na kwa namna ya pekee viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaoshiriki katika mkutano huo wanapaswa kuhakikisha kwamba wanajifunga kibwebwe ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kupambana na umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi na mapambano dhidi ya umaskini ni chanda na pete ni mambo yanayokwenda pamoja.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa mwanga wa Roho Mtakatifu ili aweze kuwangazia ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya mafao ya familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu pia amekumbusha kwamba, tarehe 7 Desemba 1965 katika mkesha wa kuhitimisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Papa Paulo VI na Patriaki Atenagora wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli walitia sahihi Tamko la pamoja lililoondoa matamko ya kutengana kati ya Makanisa haya mawili, utengano uliotokea mwaka 1054. Hili ni tukio la kihistoria katika mchakato wa upatanisho ambalo limeyawezesha Makanisa haya mawili kuanza tena majadiliano ya kiekumene katika upendo na ukweli.

Baba Mtakatifu Francisko analikumbuka tukio hili katika mkesha wa uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa Wakristo imara, hakuna hija ya kweli katika majadiliano ya kiekumene bila kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu sanjari na kuombana msamaha wao wenyewe kutokana na dhambi ya utengano. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkumbuka katika sala zao Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Mapatriaki wakuu wa Makanisa ya Mashariki ili kwamba, uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox ujengeke katika msingi wa upendo wa kidugu!

Baba Mtakatifu pia amewakumbuka wenyeheri wapya: Michele Tomaszek na Zbigniew Strazalkowski, watawa wa Shirika la Mtakatifu Francisko pamoja na Alesandro Dordi, Padre kutoka katika Shirika la Zawadi ya Imani, “Fidei Donum” waliouwawa kutokana na chuki za kidini kunako mwaka 1991. Uaminifu wa wenyeheri hawa katika kumfuasa Kristo Yesu, uwatie nguvu waamini wote lakini zaidi Wakristo wanaoteseka na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia, ili waweze kuwa na ari ya kumshuhudia Kristo kwa njia ya ujasiri wa Kiinjili. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia waamini wote maandalizi mema kwa ajili ya uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.