2015-12-07 08:44:00

Papa mstaafu Benedikto XVI kushiriki katika uzinduzi wa Mwaka wa huruma ya Mungu


Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na ufunguzi wa Lango Takatifu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne, tarehe 8 Desemba 2015, Papa mstaafu Benedikto wa XVI anatarajiwa kushiriki kikamilifu pamoja na viongozi wengine wakuu wa Serikali kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao ni Rais Sergio Mattarella wa Italia, wengine ni wakuu wa nchi na ujumbe wao kutoka Jamhuri ya Watu wa San Marino, Jamhuri ya Watu wa Czech pamoja na Ujerumani.

Baba Mtakatifu Francisko katika nyaraka na mahubiri yake kwa nyakati tofauti amekuwa akimnukuru Papa mstaafu Benedikto XVI kwa kukazia umuhimu wa  huruma na ukweli, hususan wakati wa kufungua maadhimisho ya Sinodi ya familia yaliyyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Kanisa linahamasishwa kuhakikisha kwamba, linatekeleza utume wake katika ukweli na uaminifu kwa Injili ya Kristo.

Ukweli ni dhana inayomlinda mwanadamu dhidi ya vishawishi vinavyotaka kumtumbukiza katika ubinafsi na majanga ya maisha. Bila ya ukweli, upendo unaweza kushupaa na kuwa tupu na kwamba, upendo huko hatarini katika ulimengu mamboleo ambamo ukweli unapindishwa kwa masilahi ya wachache wenye nguvu! Wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya Sinodi ya familia, Baba Mtakatifu Francisko alikaza kusema huruma ni kiini cha Ujumbe wa Injili na kwa hakika ni jina la Mungu.

Maisha na utume wa Kanisa una ambata huruma ya Mungu ambayo Mwenyezi Mungu anamkirimia mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Familia ya binadamu haina budi kuambata upendo unaojikita katika huruma, ili waweze kuwa na maisha tele. Baba Mtakatifu Francisko wakati akitangaza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapo tarehe 13 Machi 2015 alilitaka Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kuwa shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, kwa kuambata toba na wongofu wa ndani; upendo na msamaha.

Kwa kipindi cha mwaka mzima yaani kuanzia tarehe 8 Desemba 2015 hadi tarehe Sherehe ya Kristo Mfalme, mwisho wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa hakika huruma ya Mungu itakuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa zima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.