2015-12-07 09:08:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani!


Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 6 Desemba 2015 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kujifunza kutoka katika shule ya Yohane Mbatizaji anayewaalika watu kutubu na kumwongokea Mungu na hata kama wamekwisha kubatizwa ili kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Yesu Kristo. Huu ni mwaliko wa kusamehe na kusahau kama alivyofanya Yesu mwenyewe kwa wale wote wanaoomba msamaha.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi sana kutokana na ubinadamu watu kusamehe na badala yake, watu wanaendekeza tabia ya kulipizana kisasi. Ni mwaliko wa kushirikiana na wale wote wanaolia na kuomboleza; wanaofurahi na kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake. Wongofu uwasaidie waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa imani wanaoiungama na kuimwilisha katika maisha yao ya kila siku: kwa ujasiri bila kuionea aibu Injili ya Kristo. Kutokana na hali na mazingira kama haya ndiyo maana waamini kwa namna ya pekee kabisa, wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mungu ili kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata leo hii sauti ya Yohane Mbatizaji inaendelea kusikika katika Jangwa la mioyo ya wanadamu. Watu ambao wamejifungia katika ubinafsi wao, wakiwa na mioyo migumu kama jiwe, ili waweze kuanza mchakato unaowaelekeza kwenye njia mpya ya maisha mintarafu mwanga wa Injili. Huu ni mwaliko wa kuandaa miyo, tayari kupokea wokovu unaoletwa na Mwenyezi Mungu anayetaka kila mwanadamu aweze kuwa huru dhidi ya dhambi na mauti.

Ikumbukwe kwamba, wokovu ni zawadi ya Mungu kwa binadamu wote na wala hakuna mtu awaye yote anayetengwa na zawadi ya Mungu. Hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba, ni mtakatifu, mkamilifu na amekwisha okoka. Kila wakati, waamini wanahamasishwa kupokea wito wa wokovu, lakini kwa namna ya pekee kabisa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.Mungu anataka kila mtu aokoke kwa njia ya Yesu Kristo, mkombozi wa dunia.

Waamini wanaendelea kuhamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuwavuta na kuwatangazia wengine Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwafungulia mlango wa maisha mapya. Ole wake yule ambaye atashindwa kutangaza Injili aliwahi kusema Mtakatifu Paulo. Kila wakati waamini wanapomkimbilia Kristo Yesu anawajalia uwezo wa kubadilika na kuwa wema zaidi, changamoto kwa waamini kumshuhudia katika medani mbali mbali za maisha.

Mwaka huu iwe ni fursa ya kuamsha imani kwa wale wanaosinzia ili waanze tena kuonesha upendo wao kwa Yesu. Waamini wawe na ujasiri wa kuvunja milima na mabonde ya kiburi, chuki, uhasama, wivu na uvivu katika maisha. Bikira Maria awasaidie waamini kutekeleza dhamana hii kwa moyo mkuu kwa kuvunjilia mbali vikwazo na vizingiti vinavyokwamisha mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukutana na Kristo Yesu anayehitimisha ukamilifu wa matumaini ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.