2015-12-07 11:29:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha kubomoa kuta za utengano!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, kwa kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa kuwasaidia jirani kwa njia ya matendo ya huruma; tayari kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai. Ni mwaliko wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, tayari kuanza maisha mapya yanayojikita katika sala, tafakari na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji.

Hii ni changamoto inayotolewa na Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, Italia, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya uzinduzi na hatimaye maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu yanayoongozwa na kauli mbiu “Iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni”. Waamini katika hija yao ya maisha ya kiroho, wakimbilie katika kisima cha maji ya uzima, ili waweze kutakaswa na dhambi zao; waonje huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kuimarishwa katika safari yao kwa chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, yaani Ekaristi Takatifu.

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kiwe ni kipindi cha kuhamasisha moyo wa Ibada na maisha ya Kisakramenti, ili kuweza kuamsha kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwani kwa njia ya kuambata rehema na neema ya Mungu, waamini wanaweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa na jamii inayowazunguka, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko ametangaza Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu kuwa ni wakati muafaka kwa Kanisa kushuhudia na kumwilisha huruma ya Mungu katika utume na vipaumbele vyake. Ni wakati wa kuangalia madonda yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, tayari kuyaganga na kuyaponya kwa njia ya matendo ya huruma sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati; Mwenyezi Mungu na mwanadamu wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Ni wakati wa kuomba na kutoa msamaha, ili kuonja kweli upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Ni mwaliko wa kuondokana na dhambi pamoja na ubinafsi, tayari kuwasaidia na kushirikiana na wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu. Huu ni wakati kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II wa kukumbatia Fumbo la huruma ya Mungu, kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kuachana na matendo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ulimwengu wa utandawazi unaonesha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini kwa bahati mbaya anakaza kusema Kardinali Bassetti, kuna watu wanaokabiliwa na saratani ya mmong’onyoko wa maadili na utu wema; watu ambao wanaenemelewa na utamaduni wa kifo pamoja na kutumbukizwa katika utumwa mamboleo unaokiuka haki msingi za binadamu na utawala bora. Umefika wakati wa kusimama kidete kuchuchumilia mafao, maendeleo na ustawi wa wengi; mambo yanayojikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

Waamini wajitahidi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo inayoponya na kukomboa! Wawe ni wajenzi na vyombo vya majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuvunjilia mbali kuta zinazowatenganisha watu kwa misingi ya kidini, kikabila au mahali anapotoka mtu! Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni wakati muafaka wa kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya watu wake! Hii ndiyo Habari Njema ya Furaha na Matumaini kwa wale waliokata tamaa.

Ni wakati wa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa njia ya ushuhuda, majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana na kuheshimiana; kwa kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa hakika Jubilei ya huruma ya Mungu ni ujumbe wa upendo. Waamini wanachangamotishwa kutoka kifua mbele, tayari kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika matendo na uhalisia wa maisha unaojikita katika huruma ya Mungu.

Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi ya kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kama walivyokaza kusema Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Familia za Kikristo ziwe kweli ni kielelezo cha upendo, huruma, msamaha na ukarimu; shule ya kwanza ya haki, amani na mshikamano; mahali pa kukuza na kudumisha Injili ya uhai na daraja la kukutana na Mwenyezi Mungu muumba wa vyote; kukutana na Yesu Kristo, Mkombozi wa dunia na Roho Mtakatifu anayeendelea kulitakatifuza Kanisa.

Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa ya kushikamana katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji, wagonjwa, maskini na yatima. Ni wakati wa kuwasaidia walioathirika kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na ulevi wa kupindukia, ili wote hawa waonje kweli huruma ya Mungu katika maisha yao. Kardinali Gualtiero Bassetti anasema Jubilei ni kipindi cha kuonesha mshikamano katika upendo; kwa kuwajibika barabara katika majukumu ya Kikanisa na Kijamii. Wanasiasa watambue kwamba, uongozi ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Huruma ya Mungu iwakumbatie na kuwaambata wote, ili waweze kuonja upendo wa Mungu kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.