2015-12-07 12:05:00

Huruma ya Mungu ni chimbuko la maisha ya Kikristo!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusiana na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, huruma ni sifa mahususi za Mungu inayojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huruma ya Mungu inagusa undani wa maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anakaza kusema, Fumbo la Pasaka ni zawadi kubwa ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu inayojikita katika upatanisho kati ya Mungu na binadamu na kati ya binadamu wenyewe. Huruma ya Mungu ni chimbuko la maisha ya Kikristo. Jimbo kuu la Mwanza katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linataka kurudi katika chimbuko na asili ya maisha ya Kikristo, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu. Waraka wa Baba Mtakatifu Uso wa huruma umetumika kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kuwaimarisha Wakristo, tayari kuonja mwanzo mpya na upatanisho, zawadi ya Mungu kwa binadamu!

Ifuatayo ni sehemu ya barua ya kichungaji kutoka kwa Askofu mkuu Ruwa’ichi kwa Familia ya Jimbo kuu la Mwanza katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Tarehe 13 Machi 2015, alipokuwa akiadhimisha mwaka wa pili wa kuchaguliwa kwake kuwa Papa, Baba Mtakatifu Francisko alitangaza azma yake ya kuadhimisha Jubilei Maalum ya Huruma ya Mungu. Amefanya hivyo akisukumwa na mwono na uelewa sahihi wa kichungaji. Hatimaye, tarehe 11 Aprili 2015, Baba Mtakatifu alitoa hati rasmi inayojulikana kwa jina la “Misericordiae vultus”, yaani “USO WA HURUMA”. Katika hati hiyo, Baba Mtakatifu Francisko anatupatia ufafanuzi wa kiteolojia wa dhana ya huruma. Zaidi ya hayo, anatoa mtiririko mzima wa jinsi Mwaka wa Jubilei ya Huruma unavyopaswa kuadhimishwa.

Ninamwalika kila mmoja na wote kwa pamoja kulipokea tangazo hilo kwa moyo mkunjufu na wa shukrani. Aidha ninamwalika kila mwanakanisa na mtu yeyote mwenye mapenzi mema, kujipanga vema ili ashiriki vizuri na kufaidika na maadhimisho yanayohusu Mwaka wa Huruma ya Mungu. Ili kufanikisha uelewa na ushiriki wa adhimisho la Mwaka wa Huruma ya Mungu, ninaaagiza kwamba: Kila padre, shemasi, katekista na kiongozi wa halmashauri ya walei, asome kwa makini kijitabu cha “Uso wa Huruma”, ili aweze kuwasaidia wanakanisa wengine ipasavyo. Kila Jumuia ndogo-ndogo ya Kikristo ijipatie nakala za kijitabu cha Uso wa Huruma na kukisoma hatua kwa hatua katika mtiririko wa Mwaka wa Huruma ya Mungu. Aidha, kila wanapokusanyika, wanajumuia wasali Sala maalum aliyoitunga Papa Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu. Wajipange pia kujipatia fursa ya kusali Rozari ya Huruma ya Mungu na Novena ya Huruma ya Mungu.

Mahubiri na katekesi sahihi na ya kina viandaliwe ili  kuwasaidia wanakanisa kusameheana na kupatana, kupokea huruma ya Mungu tunayozawadiwa bure, kutekeleza matendo ya huruma kwa furaha na ukunjufu (kwa wagonjwa, wadhambi, waregevu wa imani, maskini, wafungwa, wapweke, wanaoonewa na kusetwa n.k.), kuielewa na kuiishi sala ya Bwana – “Baba Yetu” – hasa kile kifungu kisemacho: “Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi wale waliotukosea!!!”.

Wakristo wafundishwe kujichunguza nafsi na kisha, wakisukumwa na toba ya kweli, wakimbilie kwenye kiti cha Huruma ya Mungu, yaani cha Kitubio ili kuungama, kushauriwa na kupatanishwa na Mungu, pia na wenzao, nafsi zao na mazingira wanamoishi. Mapadre waweke kipaumbele zaidi katika utume wa kuwaganga na kuwatibu waamini kwa kuadhimisha vema zaidi, kwa ukarimu, huruma na upendo wa kichungaji – Sakramenti ya Upatanisho au Kitubio. Katika mwaka wote wa Huruma ya Mungu, Mapadre wanaruhusiwa kuondolea dhambi zilizozuiliwa. Wafanye hivyo kwa unyofu, ukomavu wa kichungaji, huruma na hofu ya Mungu. Katika Mwaka wa Huruma ya Mungu, Picha maalum ya Yesu chimbuko la itazungushwa katika Parokia zote za Jimbo Kuu la Mwanza. Zoezi hilo lifanyike kwa heshima, uangalifu na uchaji wa hali ya Juu. Mafundisho bayana yatolewe kuhusu uhusiano kati ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristu na swala la Huruma ya Mungu.

Bila shaka, katika hija ya Picha ya Huruma ya Mungu katika maeneo ya parokia, jumuia, na familia, waamini na watu wenye mapenzi mema, zitakuwepo fursa kwa  waamini na watu wenye mapenzi mema kutoa matoleo na sadaka zao kwa kadiri watakavyoguswa. Ninaagiza kwamba matoleo hayo yapokelewe kwa shukrani, heshima, uaminifu na uchaji. Aidha nusu ya matoleo hayo yatumike katika Parokia husika na nusu iwasilishwe katika ofisi za jimbo kwa kusaidia utume wa kijimbo. Wakati wote wa mwaka wa Huruma ya Mungu, waamini wasali binafsi, kifamilia, kijumuia na hata katika mikusanyiko mingine sala maalum iliyotungwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa lengo hilo. Ifuatayo ni tafsiri ya sala hiyo:

 

“Ee Bwana Yesu Kristu, umetufundisha na kutuagiza tuwe na huruma kama Baba wa mbinguni alivyo na huruma. Pia, umetufundisha kwamba anayekuona wewe, amemwona Baba! Tuonyeshe uso wako, nasi tutaokokolewa! Mtazamo wako wa huruma ulimnasua Zakayo na Matayo kutokana na utumwa wa fedha; yule mwanamke mzinzi na Maria Magdalena kutokana na utumwa wa kutafuta raha kutoka kwa viumbe, na pia mtazamo huo wa huruma ulimchoma Petro hata akalia kwa majuto baada ya kukukana; na tena, mtazamo huo wa huruma ulimhakikishia paradiso, yule mwizi aliyetubu. Tujalie kufarijiwa na yale maneno uliyomtamkia yule mwanamke msamaria ulipomwambia: ‘kama tu ungaliitambua zawadi ya Mungu!’

Ee Bwana Yesu, wewe ni uso unaoonekana wa Mungu asiyeonekana, Mungu anayedhihirisha uwezo wake hasa kwa njia ya huruma na msamaha. Lijalie kanisa lako lipate kudhihirika zaidi kuwa ni uso wako unaoonekana katika ulimwengu unaohitaji kukutambua kama Mfufuka na Mtukufu. Wewe uliridhia kujiteulia mawakili, wahudumu wa kanisa walio wadhaifu, ili waweze kusukumwa kuwahurumia wale wanaosakamwa na ujinga na makosa. Jalia kwamba yeyote anayewaendea hao mawakili wako, ahisi kuwa anatafutwa, kupendwa na kusamehewa na Mungu.

Tunakusihi umpeleke Roho wako Mtakatifu na umweke wakfu kila mmoja wetu kwa mpako wa Roho huyo, ili jubilei hii ya Huruma iwe kwetu mwaka wa neema itokayo kwa Bwana. Nalo kanisa lako, likijawa mwamko mpya, liwapelekee maskini habari njema, litangaze uhuru kwa wafungwa na walioonewa na kuwarudishia vipofu uwezo wa kuona tena. Haya tunakuomba Ee Bwana Yesu, kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Huruma.  Unayeishi na kutawala pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, milele na milele – amina.”

Napenda kuwafahamisha pia kwamba ofisi ya Baba Mtakatifu imetoa wimbo rasmi wa kusindikiza maadhimisho ya jubilei ya Huruma ya Mungu. Ifuatayo ni tafsiri ya wimbo huo: Kiitikio: Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni Mwema, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ameiumba nchi kwa hekima, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Anawaongoza watu wake katika mapito ya historia, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Anawasamehe na kuwakaribisha watoto wake, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Mshukuruni Mwana wa Mungu, Mwanga wa mataifa. Kwa maana fadhili zake zadumu milele.  Ametupenda kwa ‘moyo wa nyama’ Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Kama tunavyotunukiwa naye, nasi pia tumrudishie, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mioyo radhi kwa wote wenye njaa na kiu, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Tumsihi Roho atumiminie vipaji vyake saba, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Chimbuko la wema wote na faraja tamu kabisa, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Kama tunaofarijiwa naye, sisi nasi tuwafariji wenzetu, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Upendo huvumilia yote, hustahimili yote, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Tumwombe Mungu, asili ya amani yote, atujalie amani, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Dunia ina kiu ya Habari Njema ya Ufalme, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Furaha na msamaha mioyoni mwao walio wanyofu, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mbingu na dunia vitafanywa upya, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Ninawaalika wataalam wa muziki kuandaa tungo za kufaa, ili tuwe na nyimbo nzuri zinazotokana na mashairi hayo hapo juu. Uzinduzi wa Mwaka wa Huruma ya Mungu Utafanyika kama ifuatavyo: Mkesha wa Uzinduzi: tarehe 8 Desemba 2015 katika Madhabahu ya Kawekamo. Jioni hiyo, kutakuwa na maungamo, mada mahususi, kuabudu Ekaristi takatifu, filamu ihusuyo huruma na upatanisho. Misa Kuu ya Uzinduzi wa Mwaka wa Huruma ya Mungu itafanyika katika Madhabahu ya Kawekamo tarehe 9 Desemba 2015. Wahusika wanaopaswa kushiriki ni mapadri, watawa na waamini walei kutoka Parokia zote na asasi za kikanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.