2015-12-05 09:57:00

Tathmini kuhusu maisha na utume wa Wakleri kwa nchi za AMECEA


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika amekazia kwa namna ya pekee kwa Wakleri na Watawa: kuambata kumbu kumbu, uaminifu, sala sanjari na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji mkuu, wakitambua kwamba, wao pia wanapaswa kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa kukimbilia huruma na upendo wake kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Wakleri wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake pamoja na kuendelea kukua katika utakatifu wa maisha, ili waweze kuwa kweli ni sauti ya Kinabii kati ya watu wanaowahudumia na kuwaongoza. Dhamana hii inahitaji sala, malezi endelevu ya kiakili na kiroho; kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika huduma zao, ili kweli Wakleri waweze kuwa ni mashuhuda wa haki, amani, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Wakleri watambue kwamba wao ni wachungaji na viongozi wa Jumuiya zao, changamoto ya kuishi katika ukweli na furaha kwa kutekeleza dhamana na majukumu yao ya Kikuhani yanayojikita katika utii, usafi na useja, tayari kumfuasa Kristo pasi na kujibakiza kwa kuhakikisha kwamba, miili, akili na mioyo yao inaelekezwa kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake; mambo yanayohitaji maamuzi magumu katika maisha.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA kwa kutambua umuhimu wa malezi awali na endelevu katika maisha na utume wa Wakleri, hivi karibuni kwa kushirikiana na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji limefanya tathmini kuhusu ufanisi wa huduma na utume wa Kipadre kwa nchi za Afrika Mashariki na kati. Katika tathmini hii, wajumbe wamepembua kwa kina na mapana utambulisho wa Padre Mwafrika!

Hapa wajumbe wamegundua kwamba, Wakleri wanaweza kutambuliwa kama Mapadre wa Jimbo au Mapadre watawa; hapa mwono na vipaumbele vyao vinatofautiana kutokana na malezi awali na endelevu kwa kila kundi. Karama ya Mashirika inawasaidia Mapadre watawa kuwa na utambulisho makini katika huduma na maisha yao ikilinganishwa na Mapadre wa Jimbo. Msingi wa maisha ya familia wanamotoka Wakleri una umuhimu wa pekee katika malezi na makuzi ya Wakleri na hata maisha yao kwa siku za usoni.

Walezi wawe makini katika kuteuwa vijana wanaotaka kujiunga na wito pamoja na maisha ya Kipadre na kwamba, Familia ya Mungu iwe mstari wa mbele katika malezi na majiundo ya vijana kwenye: Familia, Jumuiya ndogo ndogo na vyama vya kitume katika maeneo yao. Mwaka wa mapumziko, warsha, semina, mafungo na makongamano ni mambo muhimu yanayoweza kuwasaidia Wakleri kutekeleza dhamana na wito wao wa Kipadre ndani ya Kanisa na Jamii inayowazunguka kwa kuonesha ukomavu wa maisha ya kiroho na kiutu!

Askofu Joseph Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma anawataka Wakleri kuchukulia changamoto za maisha na utume wa Kipadre kuwa ni sadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wawe tayari kuungana na Kristo katika furaha, mateso na magumu ya maisha wanapowahudumia watu wake, kwa kutambua kwamba, Kristo yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali na wala hatawaacha kamwe!

Wakleri wajenge utamaduni wa kuwa karibu na Kristo Yesu kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti, hususan sakramenti ya Upatanisho ili kweli waweze kuwa vyombo makini vya huruma na upendo wa Mungu, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Wakleri wanapojikuta wakiogelea na kupiga mbizi kwenye dimbwi la dhambi, wamkumbuke Mwana mpotevu na Baba mwenye huruma anayewasubiri daima kuwapokea na kuwakumbatia, tayari kuwaonjesha huruma na upendo unaokoa na kuponya!

Askofu Mlola anakaza kusema, Mapadre wanapokuwa Bondeni kwenye machozi, wanapaswa kusaidiana na kusindikizana kwa njia ya sala na ushauri makini, kwani wanafahamiana vyema zaidi kuliko hata Maaskofu wao! Wakichukuliana katika upendo, haki na huruma, wanaweza kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.