2015-12-04 08:40:00

Utunzaji bora wa mazingira na huduma makini kwa maskini ni muhimu!


Mama Kanisa anaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati unaotekelezeka katika utunzaji bora wa mazingira mintarafu Waraka wa kichungaji uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, “Laudato si”. Dhamana hii inaendelea kuvaliwa njuga na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani akishirikiana na Kardinali Oscar Andrès Maradiaga, Rais mstaafu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.

Viongozi hawa wanaendelea kuonesha mambo msingi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuweza kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, mambo yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini na magonjwa. Lengo ni kuwawezesha viongozi wa kimataifa katika mkutano wao kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi unaofanyika mjini Paris, Ufaransa kuanzia tarehe 28 Novemba hadi tarehe 11 Desemba 2015.

Kardinali Peter Turkson hivi karibuni akiwa kwenye Chuo kikuu cha George Town, Washington DC, amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza katika utunzaji bora wa mazingira sanjari na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwani hawa ndio waathirika wakuu wa athari za mabadiliko ya tabianchi. Kila nchi inapaswa kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika kuibua na kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyuba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Turkson akiwa Chuo kikuu cha Columbus, huko Ohio amepembua kwa kina na mapana mambo msingi yanayojadiliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, Laudato si. Huu ni waraka unaojikita kwenye majadiliano katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ni majadiliano yanayomgusa mtu mmoja mmoja, taasisi na jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, binadamu amekuwa ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira na kwamba, kuna haja ya kuwa na wongofu wa kiekolojia, tayari kuibua na kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Ni mchakato unaojikita katika mabadiliko ya tabia ya binadamu pamoja na kutambua kwamba, binadamu na viumbe hai wote wanategemeana na kukamilishana, kwani wanapata hifadhi katika nyumba ya wote. Kwa kuwa na mwelekeo kama huu, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuibua mbinu mkakati na sera makini katika utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Kardinali Turkson anasema, Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya utunzaji bora wa mazingira ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa na wala si kwa ajili ya “kuwapigia debe” wanaharakati wa mazingira duniani. Ni waraka unaojikita katika mafundisho ya kijamii kwa kugusa utu na heshima ya binadamu; haki, amani na maendeleo ya wengi; pengo kati ya matajiri na maskini na madhara yake katika jamii; umaskini pamoja na uchu wa mali na madaraka; mambo ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu pamoja na mazingira.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa dhati, huku wakiongozwa na kanuni auni sanjari na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa linatambua kwamba, kazi ni utumilifu wa utu na maisha ya binadamu, kumbe kuna haja ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi hili watu wengi waweze kupata fursa za ajira. Mambo yote haya yanapaswa kujadiliwa katika ukweli na uwazi bila ya kutumbukia katika kishawishi cha kukumbatia mafao ya mataifa binafsi, bali kwa kuongozwa na kanuni ya upendeleo kwa maskini na wale wote wanaoishi pembezoni mwa jamii.

Uchambuzi kama huu pia umefanywa na Kardinali Peter Turkson kwenye Chuo Kikuu cha Saint Clara, kilichoko Califonia, kwa kushiriki katika kongamano lililojikita katika majadiliano ya matumizi bora ya bonde la Silicon kama utekelezaji makini wa Waraka juu ya utunzaji bora wa mazingira, Laudato si! Mabadiliko makubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mfumo wa digitali yamepelekea mafao makubwa kwa binadamu lakini pia uharibifu wa mazingira.

Kimsingi, viongozi mbali mbali wa Kanisa wanaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuhusu umuhimu wa Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si! Waraka ambao ukitekelezwa kwa makini katika uhalisia wake, dunia itaweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Athari za mabadiliko ya tabianchi na umaskini ni sawa na chanda na pete! Jumuiya ya Kimataifa isipojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mapambano dhidi ya umaskini na magonjwa yanaweza kugonga mwamba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.