2015-12-04 07:51:00

Ujumbe wa Papa kwa Mkutano wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Uinjilishaji wa watu


Alhamisi Baba Mtakatifu Francisko majira ya asubuhi, akiwahutubia washiriki wa Mkutano wa XIX wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Uinjilishaji wa Watu, alisema Afrika inahitaji ukaribu zaidi wa Kanisa kwa ajili ya kuponya  waliojeruhiwa kiroho, kihali,wanaosubirishwa kutokana wa imani yao kwa Kristo. Na hivyo amesisitiza kwamba huu ni wakati muafaka kwa Kanisa kutoka nje na kwenda kuhubiri Injili ya upendo kwa watu wote bila kubakiza mahali. Aliutaja wakati huu kuwa ni wakati nyeti kwa ajili ya kutazama uhai zaidi wa kanisa kwa siku zijazo.

Papa alitoa maelezo hayo huku akiirejea ziara yake ya kitume aliyoikamilisha Jumatatu ya wiki hii, akieleza kile alichojionea mwenyewe, umotomoto wa kiroho na kichungaji kwa makanisa mengi machanga  Barani  Afrika, licha ya uwepo matatizo makubwa yanayokabili idadi kubwa ya wakazi wa Afrika.  Papa Francisko ameeleza kuwa katika ziara hii, iliyokuwa ya kwanza kwake kufika Afrika,  ameweza jifunza kwamba ,  Afrika inahitaji uwepo wa karibu, wa Kanisa, katika maana ya kuwa na huduma nyingi za matendo ya huruma , kwa ajili ya kukuza ubinadamu, usamaria mwema na kufanya kazi  kitume bila kuchoka. .

Katika hotuba yake, pia Papa alionya kwamba, ni lazima kurejea asili kazi za Kanisa katika kueneza injili, ambazo hudai kwanza, kuanzia ndani ya Kanisa lenyewe, ambao ni wafuasi wake, kusikiliza Neno la Mungu na kuwa na matumaini  yasiyo tahayari kwa kuwa yamejengwa juu ya neema ya Roho Mtakatifu (Rum 5.5). Na hivyo ni  kwa namna hiyo tu , inawezekana kuwa na uwezo wa kudumisha upya  utendaji wa Kitume. Papa alirejea pia Azimio la Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, juu ya  Utume wa Kanisa kwa Watu “Ad Gentes” na Waraka wa Kipapa wa Utume wa Kukomboa , “Redemptoris Missio” akisema bila shaka Mkutano unaoendelea unafanyika kwa uvuvio wa nyaraka hizo, kwa dhamira ya Mwana na ujumbe wa Roho Mtakatifu kwa  Kanisa, kulingana na mpango wa Mungu Baba, ambaye ni asili yake.

Papa aliendelea kutaja lengo la kazi za Utume wa Kanisa huduma za kitume akisema ,zinapaswa kufanyika si katika nguvu za mipango ya binadamu; lakini mtendaji wake mkuu anapaswa kuwa Roho Mtakatifu, na ni mfanikishaji wa utume huo, kama ilivyokuwa tangu mwanzo wake , hata leo huu. Kumbe katika ukweli wake, si Kanisa linalofanya kazi za kitume , bali ni nguvu za Roho Mtakatifu zenye kuunda Kanisa . Na utume si kama chombo lakini ni hatua ya mwanzo na mwisho.

Papa alieleza na kurejea barua ya Shirika ya hivi karibuni, iliyorejea takwimu za utafiti juu ya uhai wa Makanisa Machanga kwa ajili ya kupata mawazo mapya  yanayofaa zaidi katika kuchukua hatua makini zaidi kwa ajili ya ufanisi zaidi katika kazi za kutangaza  Injili katika mataifa na katika kukabiliana na  utata na changamoto zinazokabili mataifa mengi yenye uzoefu wa  imani kwa karne nyingi. Papa alisema, katika  Ulimwengu wa kidunia, kwa kweli, hata kama  kuna joto  la maadili  ya Kiinjili katika  upendo, haki, amani na moyo wa kiasi, hapawezi onyesha kwa uwazi Utu wa Yesu, wala kuwa na fikira kama ni Masihi wala Mwana wa Mungu , kwa kuwa hilo linahitaji mtu aliyeangaziwa na kuwa na upeo katika macho ya Imani.

 Hivyo kumbe ni  muhimu, Papa alisisitiza katika wakati huu Kanisa ni lazima kutoka nje, kwenda  kutangaza injili kwa watu wote, katika maeneo yote, katika wakati wote, bila kuchelewa, wala bila kujihurumia na bila  hofu (ibid., N. Evangelii Gaudium, 23).  Ni kutenda kwa nguvu za kudhamiria , kwa ajili ya  kuleta mabadiliko ndani ya Kanisa lenyewe kwanza, na hatimaye katika  maisha ya watu na tamaduni.  Hotuba ya Papa , imetoa wito kwa  kila Parokia kupania kuivaa sura na mtindo huu wa kutoka  nje na kwenda kutangaza habari njema ya Injili kwa mataifa. Na ili kuweza kufanikisha hili ni lazima kuzama katika maombi ili Roho Mtakatifu ayabadili maisha ya waumini, wakichukua tabia ya  wanafunzi wa  Yesu,  wanafunzi waliopata ambukizo la kutenda kazi za kitume, zenye kuwaunganisha pamoja bila hofu, wala kujifungia ndani lakini  wenye kujionyesha waziwazi  pande zote, hata miisho ya dunia.  Papa alitaja hiyo ndiyo mbinu ya kuitangaza Imani, na pia kama hatua ya kufanikisha nafasi kwa familia ya makanisa machanga kuwa na nafasi pia ya kutoa huduma katika Makanisa ya kale. Papa alieleza na kuomba kazi za Utume wa Kanisa ziendelee kufanyika katika misingi ya Matendo ya Mitume.

Ameomba  maongozi ya nguvu ya Injili na Roho Mtakatifu na si kukurupuka kwa nguvu zetu za kibinadamu,  ambamo pia wakati mwingine mna majaribu ya sisi wenyewe kwa wenyewe. Na pia akaomba msaada wa. Mtakatifu Maria, Mama wa Mungu, Mtakatifu Francis Xavier na Mtakatifu Therese wa Mtoto Yesu, mlinzi wa ujumbe, waangazie  njia  katika utumishi wa Injili ya Bwana Yesu.  Na kwamba, katika mkutano huu anaongoza nao na akawapa Baraka zake za kitume na pia kuwaomba sala zao.

Katika Mkutano huu wa XIX, miongoni mwa washiriki wake ni Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa ya Haki na Amani. Naye   akizungumza  juu ya Makanisa Machanga, awali ya yote alibainisha kuwa, katika nyakati hizi, katika maisha ya Kanisa katika kazi ya kutangaza Injili, hukutana na vipingamizi vingi vyenye kudhoofisha juhudi za  uinjilishaji,  kutokana na hali halisi za mazingira, kijamii na kitamaduni  pia. Pamoja na changamoto hizo, pia aliutaja upende wa pili wenye kuonyesha mafanikio kaika ongezeko la waumini katika makanisa machanga akisema ni wazi idadi inayoongezeka ni jambo la kuvutia na kuwa na matumaini  katika  baadhi ya maeneo.  Kipengele kingine kilichosisitizwa na Rais wa Baraza la  Haki na Amani, ni juu ya umuhimu wa mchango unaotolewa na Makanisa machanga katika utumishi wa Mapadre majimboni na katika mashirika ya kitume, ambao huziba pengo katika nchi kongwe kwenye Ukristo kama baani Ulaya na Marekani,ambako sasa kunajionyesha kuwa na mabadiliko makubwa katika maisha ya Kanisa .  Hivyo Kardinali Turkson katika Mkutano huu aliwasilisha maswali mawili, kwa jinsi gani inawezekana kutuliza hali katika makanisa mahalia,  ili kupunguza uhamiaji unapita ; na jinsi gani uwepo wa wakimbizi barani Ulaya unaweza kuliongoza Kanisa katika kugundua  upya sauti yake ya kinabii. 








All the contents on this site are copyrighted ©.