2015-12-04 07:32:00

Sekta isiyo rasmi itaboreshwa ili ichangie zaidi katika ukuaji wa uchumi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni amesema Serikali ya Tanzania inatekeleza mikakati ya kuweka mazingira bora ili sekta isiyo rasmi iweze kuchangia vizuri katika maendeleo ya Taifa. Mhe. Magufuli aliyasema hayo wakati akifungua Maonesho ya Wajasiriamali ya Juakali/Nguvu Kazi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam. Akifungua kwa niaba ya Rais, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Said Meck Sadiki alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuweka mpango maalumu wa kurasimisha shughuli za Sekta isiyo rasmi (MKURABITA).

Alisema mpango hu unatoa fursa ya mikopo nafuu kuwawezesha wajasiriamali na kuwapa elimuya namna bora ya kufungasha bidhaa zinazozalishwa. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Said Meck Sadiki maonesho hayo yameshirikisha wajasiriamali zaidi ya 700 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Pia maonesho hayo wamehudhuriwa na Mabalozi kutoka nchi wanachama, Makatibu Wakuu,Wakurugenzi, Wenyeviti wa Wajasiriamali hao kutoka Nchi wanachama. Maonesho hayo pia yameshirikisha Taasisi mbalimbali zikiwemo Taasisi za Fedha,Taasisi ya Mifuko ya Jamii na Mamlaka ya usajili (BRELA).

Kabla ya kufungua maonesho hayo, Mheshimiwa Said Meck Sadiki alitembelea baadhi ya mabanda ili kuona kazi za wajasiriamali hao. Mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali Wasiorasimishwa Afrika Mashariki, Josephat Rweyemamu alisema madhumuni ya maonesho hayo ikiwemo kuwawezesha wajasiriamali kupanua masoko ya bidhaa zao pamoja na changamoto wanazozipata wajasiriamali hao.  Alieleza baadhi ya changamoto kuwa ni ukubwa wa kodi, pia aliiomba Serikali kufungua kiwanda cha Urafiki ili kuwasaidia wajasiriamali pia kuwatengea maeneo maalum kwa ajili ya kufanyia biashara zao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Joyce Mapunjo alieleza kufurahishwa na bidhaa za wajasiriamali. “Nimefurahishwa sana na bidhaa mbalimbali toka kwa wajasiriamali wa Afrika Mashariki na Serikali zetu za Afrika Mashariki zinatambua mchango wa Sektaisiyo rasmi na ndio mana tukawa na maonesho haya”.alisema Mhe. Dkt. Mapunjo. Hata hivyo, alisema pamoja na mafanikio hayo, Serikali za nchi wanachama zinatambua kwamba Sekta isiyo rasmi inakabiliwa na vikwazo na changamoto nyingi ambazo zinadumaza maendeleo ya Sekta hii isiweze kukuwa na kuwa Sekta rasmi.

Rais John Pombe Magufuli amewahakikishia wajasiriamali wa Tanzania kuwa wameshayajadili na kwa sasa wanayafanyia kazi. “Kuna hatua ambayo Serikali ya Tanzania inatekeleza katika kuweka mazingira bora ili Sekta isiyo rasmi iweze kuchangia vizuri katika maendeleo ya Taifa letu” aliongeza. Maonesho hayo yalianzishwa tangu mwaka 1999 na hufanyika katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mzunguko. Kwa Tanzania haya ni maonesho ya Tano kufanyika na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Nunua bidhaa zilizozalishwa na Afrika Mashariki ili kukuza uchumi wa Afrika Mashariki”.

Wakati huo huo, Serikali kupitia Kampuni Tanzu ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania, (TGDC) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Iceland (ICEIDA), wamesaini Mkataba wa Makubaliano utakaowezesha Tanzania kunufaika na msaada wa kiasi cha Dola za Marekani 1,565,000 kwa ajili ya kupata mtaalam mwelekezi kufanya tafiti katika maeneo yenye viashiria vya Jotoardhi; kuwajengea uwezo wataalam wa ndani katika tasnia hiyo ikiwemo pia kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya utafiti wa nishati hiyo. Makubaliano hayo yalifikiwa jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja na Mkurugenzi Mkuu wa ICEIDA, Engilbert Gudmundsson, ambapo tukio hilo lilishuhudiwa na Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe, Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Uendelezaji wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, baadhi ya Maafisa kutoka TGDC na Wizara ya Nishati na Madini.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Paul Masanja alisema kuwa, matarajio ya Tanzania ni kuzalisha kiasi cha megawati 200 za umeme unaotokana na nishati ya jotoardhi ifikapo mwaka 2020 ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa, hazina iliyopo kupitia nishati hiyo ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati elfu tano za umeme (5,000), kutokana na nishati ya jotoardhi . Aidha, Mhandisi Masanja aliongeza kuwa, utayari na ushirikiano iliyouonesha nchi ya Iceland kupitia ICEIDA itakuwa kichocheo kikubwa kufikia malengo ya serikali ya kuwa na nishati ya kutosha ya umeme kutoka vyanzo mbalimbali.

“Tuna malengo yetu mengi kupitia nishati hii, utafiti ndio njia itakayotufanya kufikia malengo yetu hivyo, ushirikiano huu ni mwanzo mzuri kwa upande wetu. Nafahamu Iceland mlianzia katika hatua za chini kabisa lakini sasa mko mbali. Naamini uzoefu wenu utatuwezesha kuweza kufika mahali tunapotarajia,” aliongeza Mhandisi Masanja. Aidha, Masanja aliitaka Kampuni ya TGDC, kuhakikisha inashirikiana vizuri na nchi ya Iceland ikiwemo shirika la ICEIDA kuhakikisha linafuata ushauri mzuri wa kitaalamu unaotolewa na shirika hilo ili kuweza kupata uzoefu, jambo ambalo litawezesha sekta ya jotoadhi nchini kupiga hatua na hivyo kuifanya jotoardhi kuwa chanzo kingine cha nishati ya umeme.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe, alishukuru utayari wa ICEIDA katika kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia malengo yake ya kuendeleza nishati hiyo, utayari ambao utasaidia kufanyika kwa tafiti katika maeneo yenye viashiria vya jotoardhi ya Luhoi, na Kibiti, Mkoa wa Pwani.Vilevile, Mhandisi Njombe alieleza kuwa, kutokana na utafiti utakaofanywa, utawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi ambazo zitafungua njia ya kupata msaada zaidi kutoka katika taasisi ambazo zimejikita katika masuala ya zenye uhusiano na nishati ya jotoardhi, jambo ambalo pia litawezesha uendelezaji wa nishati hiyo nchini. Aidha, Mhandisi Njombe alitumia fursa hiyo pia kueleza hatua mbalimbali ambazo tayari zimefanywa na kampuni hiyo katika kuhakikisha kwamba, jotoardhi inakuwa chanzo kingine cha uzalishaji umeme nchini na kuongeza kuwa, kupitia makubaliano hayo, ICEIDA itawezesha wataalam wa ndani wa TGDC kupata ujuzi na uzoefu utakaowezesha kufanyika kwa tafiti nyingine katika maeneo ya Kiejo/ Mbaka, Mkoa wa Mbeya.

Naye, Mkurugenzi wa ICEIDA, Engilbert Gudmundsson alieleza umuhimu wa nishati hiyo na unafuu wake wa gharama ikilinganishwa na nishati nyingine na kueleza kuwa, asilimia 25 ya umeme unaozalishwa nchini Iceland unatokana na nishati ya jotoardhi. “Ilituchukua kipindi cha miaka 25 kufikia mafanikio tuliyonayo katika nishati ya jotoardhi. Kutokana na ubobezi huu ni vema kwetu kutoa uzoefu kwa TGDC kuhakikisha inafakia malengo tarajiwa na kwamba jotoardhi inakuwa chanzo kingine cha umeme kwa Tanzania ambao ni rahisi na nafuu,”aliongeza Engilbert.

Jotoardhi ni mojawapo ya chanzo cha nishati kitokanacho na mvuke unaotoka ardhini, hususan katika maeneo yaliyo katika Bonde la Ufa (Rift Valley). Nchizilizo katika bonde la Ufa (African Rift Geothemal Facility – ARGeo) ni pamoja na Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Tayari Tanzania imefanya jitihada kadhaa za kuendeleza Jotoardhi ikiwemo uanzishwaji wa Kampuni ya TGDC, ambayo ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), iliyoanzishwa mwezi Juni, 2014. TGDC inatajwa kuwa kichocheo muhimu cha uendelezaji wa nishati ya jotoardhi. Aidha, mwishoni mwa mwezi Oktoba hadi mwanzoni mwa Novemba 2014, Tanzania ilikuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Jotoardhi uliofanyika Jijini Arusha. Mkutano wa Jotoardhi unatajwa kuinufaisha Tanzania katika kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu ili kuchangia upatikanaji wa nishati hiyo nchini; kubadilishana uzoefu na uelewa na wataalamu kutoka nchi mbalimbali duniani; ikiwemo pia kuharakisha uendelezaji wa jotoardhi.

Na mwandishi maalum!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.